1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Harakati ya 'Linda Niger' kuzinduliwa Jumamosi mjini Niamey

Zainab Aziz
16 Agosti 2023

Raia wa Niger wanajiandaa kwa vita dhidi ya nchi za kanda ya Afrika magharibi zinazotishia kuivamia nchi yao, wiki tatu baada ya wanajeshi waasi kumuondoa madarakani rais wa taifa hilo aliyechaguliwa kidemokrasia.

https://p.dw.com/p/4VE6k
Raia wa Niger wanaoliunga mkono jeshi lililofanya mapinduzi mjini Niamey
Raia wa Niger wanaoliunga mkono jeshi lililofanya mapinduziPicha: Balima Boureima/AA/picture alliance

Wakaazi katika mji mkuu wa Niger, Niamey, wanawataka watu wajitolee na kujisajili kwa wingi ili kulisaidia jeshi kutokana na kuongezeka vitisho vya Jumuiya ya Afrika Magharibi, ECOWAS, ambayo imesema inaweza kutumia nguvu za kijeshi ikiwa jeshi la Niger halitamrejesha Rais Mohamed Bazoum waliyemuondoa madarakani mnamo tarehe 26 mwezi uliopita wa Julai.

Mwito huo, unaoongozwa na kundi la wenyeji wa mji mkuu wa Niger, Niamey, wanolenga kuwasajili maelfu ya watu kote nchini wanaotakiwa kujiandikisha kwa kujitolea kuilinda Niger.

Wanatakiwa watakaopigana, watakaosaidia kwenye huduma za matibabu za kiufundi na hata uhandisi vifaa miongoni mwa huduma zingine.

Wafuasi wa jeshi lililoongoza mapinduzi nchini Niger katika uwanja wa michezo wa Niamey.
Wafuasi wa jeshi lililoongoza mapinduzi nchini Niger katika uwanja wa michezo wa Niamey.Picha: AFP

Amsarou Bako, mmoja wa waanzilishi, ameliambia shirika la Habari la Associated Press kwamba wanahitajika raia wenye uchungu na nchi yao kuwa tayari wakati wowote utakapotokea uvamizi. Harakati hiyo ya kuwasajili watu itazinduliwa siku ya Jumamosi katika mji wa Niamey vile vile katika miji ambayo inaweza kuvamiwa karibu na mipaka kati ya Niger na Nigeria na Benin, nchi mbili, ambazo zimesema zitashiriki iwapo ECOWAS itatoa agizo hilo.

Soma pia: Majenerali Niger wamrejesha nyumbani balozi wake kutoka Abidjan

Vyanzo vya kijeshi na vya kisiasa vimesema, wakuu wa kijeshi kutoka nchi za jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS watakutana nchini Ghana wiki hii kujadili uwezekano wa kuingilia kati nchini Niger.

Mkutano huo utakaofanyika siku ya Alhamisi na Ijumaa ulipangwa kufanyika wikiendi iliyopita lakini ukaahirishwa na sasa utafanyika baada ya viongozi wa ECOWAS wiki iliyopita kuidhinisha kupelekwa kikosi cha uangalizi kwa ajili ya kurejesha utulivu wa kikatiba nchini Niger.

Washiriki katika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Afrika magharibi, ECOWAS mjini Abuja, Nigeria.
Washiriki katika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Afrika magharibi, ECOWAS mjini Abuja, Nigeria.Picha: Xinhua News Agency/picture alliance

Wachambuzi wanasema uingiliaji kati wa kijeshi unaweza kuwa ni hatua ya hatari kiutendaji na pia hatari kisiasa, kwa kuzingatia mgawanyiko uliopo ndani ya safu za jumuiya  ya ECOWAS na ukosoaji wa ndani ya nchi za kanda hiyo.

Wizara ya ulinzi ya Niger imesema kwenye taarifa yake kwamba wanajeshi 17 waliuawa katika shambulizi la kuvizia la hapo jana Jumanne katika eneo la kusini magharibi  mwa Niger linalopakana na Burkina Faso.

Wakati hayo yakiendelea gharama za maisha zimezidi kupanda katika mji wa Niamey.

Wananchi wa Niger wanasema, wameanza kuhisi athari ya vikwazo vya usafiri na kiuchumi vilivyowekwa na jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS. Niger ina idadi ya watu milioni 25 na ni mojawapo kati ya nchi maskini zaidi duniani. Lakini licha ya kuwekewa vikwazo, viongozi wa kijeshi walioongoza mapinduzi wamekataa mapendekezo ya ECOWAS ya kumwachilia rais waliyemwondoa madarakani Mohamed Bazoum.

	Kiongozi wa Kijeshi wa Niamey Jenerali Abdourahamane Tiani.
Kiongozi wa Kijeshi wa Niamey Jenerali Abdourahamane Tiani.Picha: Télé Sahel/AFP

Soma pia: Utawala wa kijeshi wa Niger wasema upo tayari kwa mazungumzo

Mvutano kati ya Niger na jumuiya ya ECOWAS hauonyeshi dalili zozote za kupungua, licha ya ishara kutoka pande zote mbili kwamba wako tayari kuusuluhisha mgogoro huo kwa amani.

Wiki iliyopita jeshi lilisema liko tayari kufanya mazungumzo na ECOWAS lakini muda mfupi baadaye lilitangaza kuwa rais aliyeondolewa madarakani Bazoum atashtakiwa kwa  makosa ya uhaini.