1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila Odinga atafakari hatua za kuchukua baada ya uchaguzi

Isaac Gamba
14 Agosti 2017

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga anatafakari hatua za kuchukua huku akiendelea kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo akisisitiza  kulikuwa na udanganyifu.

https://p.dw.com/p/2iBCc
Kenia Oppositionsführer Raila Odinga im Mathare slum in Nairobi
Picha: Reuters/S. Modola

Raila Odinga mwenye umri wa miaka 72 anasisitiza ndiye mshindi katika uchaguzi huo na ametoa mwito kwa wafuasi wake kutokwenda kazini hii leo ili kuomboleza vifo vya wale waliouawa katika maandamano kupinga kutangazwa  Rais Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa nafasi ya urais huku wafuasi wa kiongozi huyo wa upinzani wakiendelea kusubiri tamko aliloahidi atalitoa kesho Jumanne kuhusiana na hatua za baadaye watakazochukua.

Hata hivyo baada ya karibu kipindi cha wiki moja  ambapo shughuli zilisimama nchini humo hali imeonekana kurejea katika hali ya kawaida katika jiji la Nairobi hii leo huku wengi wakionekana kurejea kazini na  kutokubali kuendelea kupoteza muda kwa kusalia majumbani mwao licha ya kiongozi wa upinzani kuwataka kufanya hivyo.

Mmoja wa wafanyabiashara ya matunda  katika jiji la Nairobi, Alex Kilonzo, alisikika akisema kuwa iwapo angekuwa ana pesa basi angeligoma lakini kawa sasa hawezi kufanya hivyo.

Hii ni mara ya nne kwa Raila Odinga ambaye ni mwanasiasa wa upinzani kushindwa katika uchaguzi huo na amekuwa akiendelea kusisitiza kuwa  alishinda katika chaguzi za mwaka 2007 na pia mwaka 2013.

Baada ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya mshindi wa kiti cha Rais Ijumaa iliyopita maandamano ya watu wenye hasira yalifanyika Ijumaa usiku  na Jumamosi katika maeneo ambayo ni ngome  kuu ya Odinga na  pia katika eneo la mabanda jijini Nairobi ambapo watu 16 waliuawa akiwemo msichana mwenye umri wa miaka 9.

 

Vyombo vya usalama Kenya vyakanusha kuuawa watu wasio na hatia

Kenia Charles Owino, Sprecher der Polizei und DW-Korrespondent Shisia Wasilwa
Charles Owino Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kenya akihojiwa na mwandishi habari wa DW Shisia WasilwaPicha: DW/S. Wasilwa

Polisi nchini Kenya wamekanusha kuuawa kwa waandamanaji wasio na hatia  wakidai waliouwa ni watu waliokuwa na silaha na walionekana kuwashambulia maafisa wa polisi  na waliofanya vitendo vingine vya uhalifu kama vile ubakaji pamoja na wizi.

Kenya mara kadhaa imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na mwaka 2007 wakati Odinga aliposhindwa katika uchaguzi wa mwaka huo ambao waangalizi wengi walikiri  ulikuwa na mapungufu ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.

Uchaguzi wa mwaka huu umeibua kumbukumbu ya  vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi uliofanyika muongo mmoja uliopita ambapo watu 1,100 waliuawa  huku wengine 600,000 wakilazimika kuyahama makazi yao.

Historia inaonesha kuwa marais watatu kati ya wanne nchini Kenya wanatoka katika kabila la wakikuyu huku mmoja akiwa ni mkalenjini hali inayoonesha kuyatenga  makabila mengine makubwa nchini humo kama wajaluo kushika madaraka ya urais katika kipindi cha nusu karne sasa.

Wakati hayo yakiendelea wafuasi wa mgombea wa kiongozi wa upinzani  Raila Odinga kutoka kabila la kijaluo hapo jana Jumapili katika eneo la mabanda la mathare jijini Nairobi  walipambana na wafuasi wa kundi  la wakikuyu wanaomuunga mkono Uhuru Kenyatta. Hata hivyo Japeth Koome  afisa wa polis katika jiji la Nairobi alikanusha kuwepo tukio hilo katika eneo la Mathare.

Kenia nach Wahlen Unruhen und Protest
Polisi wa kutuliza ghasia wakiwasili katika moja ya eneo mjini Kisumu. Picha: Getty Images/AFP/F. Lerneryd

 Licha  ya vurugu kuonekana kutulia wafuasi wa Raila Odinga bado wanasubiri tamko kutoka kwa kiongozi huyo huku  Odinga mwenyewe akisema hajakata tamaa na amewataka kusubiri tamko atakalolitoa hapo kesho Jumanne.

Umoja wa Mataifa, Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Ulaya wamemtaka Odinga kufuata taratibu za kisheria katika kutafuta kile anachodai. Katibu Mkuu wazamani wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan ambaye alishiriki katika kutanzua mzozo ulioibuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008 amewaonya viongozi wa kisiasa nchini Kenya kuwa waangalifu na kauli zao wanazotoa kipindi hiki.

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/ape

Mhariri: Mohammed Khelef