1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila Odinga awashauri wafuasi wake wasusie kwenda kazini

Zainab Aziz
13 Agosti 2017

Upande wa upinzani nchini Kenya washinikizwa ukubali kuwa umeshindwa kwenye uchaguzi wa wiki iliyopita huku miito kutoka ndani ya Kenya na nje inamtaka Raila Odinga akubali kushindwa kwenye uchaguzi mkuu uliomalizika.

https://p.dw.com/p/2i9JN
Kenia Wahl Politiker Raila Odinga vor Anhängern
Picha: Reuters/B. Inganga

Taarifa kutoka ofisi ya rais nchini Kenya imesema vurugu zilizotokea katika baadhi ya maeneo nchini humo zilivuka mipaka na zilikuwa kinyume cha sheria. Msemaji wa rais Manoah Esipisu amesema maandamano ya amani ni haki ya raia na kwamba polisi watatoa ulinzi kwa wananchi wakati wote. Esipisu amesema polisi hawatawavumilia watu wenye nia ya kuvuruga amani.

Kwa mara ya kwanza Odinga azungumza

Kenia Wahl Politiker Raila Odinga
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila OdingaPicha: Reuters/T. Mukoya

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amewalaumu  polisi kwa mauaji ya wafuasi wa upinzani wakati walipokuwa wanafanya maandamano kupinga matokeo ya uchaguzi.  Kiongozi huyo wa upinzani siku ya Jumapili alizungumza na umati huko Kibera eneo la mabanda katika jiji la Nairobi ambako wafuasi wa upinzani wamekuwa wanapambana na polisi ambao walifyatua risasi na pia walitumia gesi ya kutoa machozi. Odinga amewatolea mwito wafuasi wake kususia kazi siku ya Jumatatu.  Kiongozi huyo wa upinzani anasema kuna  "njama ya kuwaua wafuasi wa muungano wa NASA" na ameahidi kwamba atatoa tamko maalum siku ya Jumanne.

Vurugu katika maeneo kadhaa

Vurugu zimezuka katika baadhi ya maeneo nchini Kenya  baada ya muungano wa NASA kusema kwamba uchaguzi wa Agosti 8 uligubikwa na wizi wa kura.  Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC imesema Rais Uhuru Kenyatta alishinda uchaguzi huo na kwamba mchakato nzima wa kupiga kura haukuwa na dosari. Wakati huo huo maeneo mengi yaliyokumbwa na vurugu yameendelea kuwa na utulivu huku viongozi wa kidini wakiendelea kuwahamasisha waumini wao wadumishe amani katika maeneo ya mabanda ya Mathare.

Kenia nach den Wahlen - Graffiti in Nairobi
Bango linalohamasisha Umoja "Kenya ni zaidi ya Siasa"Picha: DW/A. Bakkar-Jalloh

Watu wauwawa kwenye vurugu

Hadi sasa jumla ya watu 16 wameuwawa kutokana na vurugu zilizozuka baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa. Idadi hiyo ni kama ifuatavyo:  Watu wanane kutoka jiji la Nairobi, wanne Kisumu, wawili Siaya, mmoja Migori na mwengine Homabay. Waziri wa mambo ya ndani na usalama wa taifa Fred Matiang'i amekanusha kuwa polisi wamewapiga risasi waandamanaji waliokuwa wanaandamana kwa utulivu bali amesema watu hao walikuwa wahalifu. Polisi nchini Kenya wamekanusha ripoti iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu nchini Kenya kwamba maafisa wa polisi wamewauwa watu 24 kufuatia vurugu za uchaguzi.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE/RTRE

Mhariri: John Juma