1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais amteua hasimu wake kuwa makamu Sudan kusini

13 Februari 2016

Rais wa Sudan kusini Salva Kiir amemteua hasimu wake mkubwa Riek Machar kuwa makamu wake katika kile kinachoelezwa kuwa uwezekano wa serikali ya Umoja wa kitaifa.na kuongeza matumaini ya amani nchini humo.

https://p.dw.com/p/1Hum1
Südsudan Salva Kiir Mayardit und Riek Machar
Rais wa Sudan kusini Salva Kiir(kushoto) akiwa pamoja na Riek Machar(Kulia)Picha: Getty Images/AFP

Rais Salva Kiir anatarajia kiongozi huyo wa waasi Riek Machar kusafiri kwenda Sudan kusini na kuwa makamu wa kwanza wa rais wa nchi hiyo , amesema msemaji wa rais Ateny Wek Ateny alipozungumza na shirika la habari la Associated Press siku ya Ijumaa(12.02.2016).

"Sioni sababu yoyote kwanini hataweza kuja mjini Juba," Ateny amesema, akimaanisha mji mkuu wa Sudan kusini. "Iwapo kuna sababu, basi itabidi aieleze dunia."

Südsudan Salva Kiir Mayardit
Rais Salva Kiir wa Sudan kusiniPicha: Getty Images/AFP/M. Sharma

Uteuzi wa Machar "hautakuwa na athari katika uundaji wa serikali," amesema james Gatdet Dak , msemaji wa Machar, ambaye amekuwa akiishi nchini Ethiopia.

Machar ataka majeshi yaondolewe Juba

"Uteuzi huo unakuja bila kutarajiwa kwasababu ya matukio mbali mbali ambayo si sahihi, lakini tumeyakubali, na uko katika njia sahihi na utekelezaji wa makubaliano ya amani," amesema.

"Ni kwamba tu umekuja katika wakati ambao si muafaka."

Akaongeza: "Tulifikiri (Machar) angewasili kwanza Juba na kisha kuteuliwa."

Utekelezaji wa makubaliano ya amani , yaliyotiwa saini mwezi Agosti, yamekwama kwasababu Kiir aliamuru kuundwa kwa majimbo 28 kutoka majimbo 10 yaliyokuwapo, na kuvuruga kifungu cha kugawana madaraka katika makubaliano ambayo yanatoa udhibiti kwa upande wa Machar wa majimbo mawili ya hapo kabla. Machar pia anataka serikali kuondoa majeshi yake kutoka Juba, kama inavyoainishwa katika makubaliano ya amani.

Südsudan Rebellenführer Riek Machar
Kiongozi wa waasi Riek MacharPicha: Reuters/G. Tomasevic

Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa jana Ijumaa (12.02.2016)umekaribisha hatua hiyo ya uteuzi na kumtaka Machar kurejea mjini Juba, msemaji wa katibu mkuu , Stephane Durarric amewaambia waandishi habari.

Mapigano ya hapa na pale yameendelea kati ya majeshi ya serikali na waasi katika baadhi ya maeneo yenye kuzalisha mafuta mashariki mwa nchi hiyo.

Machar amekuwa makamu wa Kiir hadi Julai 2013, wakati kufutwa kwake kazi kulizusha mzozo wa kisiasa ambao baadaye uligeuka kuwa uasi kufuatia mgawanyiko mkubwa miongoni mwa majeshi ya usalama mjini Juba. Baadhi ya mapigano yalikuwa katika misingi ya kikabila, na pande zote mbili zimeshutumiwa kwa kufanya uhalifu mbaya dhidi ya raia.

Darfur Kämpfer der Rapid Support Forces
Silaha bado zinaingia nchini humo licha ya vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa mataifaPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Licha ya kuwapo makubaliano hayo ya amani, pande zote mbili ziliendelea kutafuta silaha mpya , kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na jopo la wataalamu wa Umoja wa mataifa.

Jopo hilo lilisema kwamba katikati ya mwezi Septemba , serikali ya Sudan kusini ilikuwa inajaribu kupanga malipo kwa ajili ya kupata helikopta nne za mashambulizi kutoka kampuni moja iliyo na makao yake nchini Uganda , Bosasy Logistics. Waasi wamepata risasi na silaha kutoka nchi jirani ya Sudan, ripoti hiyo imesema.

Mwandishi : Sekione Kitojo / ape

Mhariri: Isaac gamba