1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Asif Ali Zardar atakiwa kujiuzulu

17 Desemba 2009

Ni baada ya Mahakama Kuu nchini humo kufuta msamaha uliokuwa ukimlinda

https://p.dw.com/p/L64S
Rais Asif Ali Zardar wa Pakistan, ambaye anatakiwa kujiuzulu.Picha: AP

Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan anakabiliwa na wito zaidi wa kumtaka ajiuzulu baada ya mahakama kuu nchini humo kufuta msamaha uliokua ukimlinda rais huyo ambaye umaarufu wake unazidi kushuka. Msamaha huo uliohusiana na mashtaka ya rushwa ulimhusu Zardari na washirika wake kadhaa. Zaidi juu ya hali hiyo na matukio mengine nchini Pakistan.

Uamuzi wa mahakama kuu ya Pakistan jana umezidisha hali ya wasi wasi katika taifa hilo lenye silaha ya kinyuklia.

Wapinzani wa rais Zardari wanapanga sasa kuhoji uhalali wake wa kuendelea kushika wadhifa huo.

Zardari binafsi pamoja na washirika wake wanasema mashitaka ya rushwa dhidi yao, yana malengo ya kisiasa na kwamba hatojiuzulu.

Wakosoaji wanasema kutokana na uamuzi huo, anawajibika kuzingatia maadili na kujiuzulu, kabla ya mahakama kutakiwa kusikiliza maombi yoyote yatakayoawasilishwa kupinga utawala wake.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu kutoka chama cha upinzani Muslim League, Bw Khawaja Asif, alisema kujiuzulu rais Zardari kutakuwa ni kwa manufaa yake binafsi, chama chake, na kwa mfumo mzima wa utawala kawa Pakistan.

Majaji 17 wa mahakama kuu wakiongozwa na Jaji mkuu Ifrikhar Mohammad Chaudry, walipitisha uamuzi huo kwa pamoja, ambao unaonekana ni pigo kubwa kwa Zardari ambaye hivi karibuni alipunguza madaraka yake makubwa aliyokuwa nayo, kwa lengo la kujaribu kupunguza pia upinzani dhidi yake.

Ingawa hakuwahi kuhukumiwa, lakini kiongozi huyo aliwahi kuwa gerezani kwa miaka kiasi ya 11 kabla ya kuachiwa huru, na baadae kufutiwa msamaha uliotokana na kanuni iliosainiwa na Kiongozi wa zamani Pervez Musharraf.

Msamaha huo wa Oktoba 2007 ulitokana na makubaliano ya kugawana madaraka kati yake na mkewe Zardari, waziri mkuu wa zamani hayati Benazir Bhutto.

Bhutto alirudi nyumbani kutoka uhamishoni Desemba mwaka huo, na akauawa baadae katika shambulio la bomu wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu.

Zardari aliteuliwa na chama chake kukiongoza na kuchaguliwa na bunge kuwa rais, baada ya ushindi wa PPP katika uchaguzi huo Februari 2008.

Changamoto inayomkabili Zardari hivi sasa imeungana na hali tete inayozidi nchini Pakistan.

Leo asubuhi shambulio la jeshi la kombora la Marekani katika kijiji cha Gadakai kilomita 35 magharibi mwa wilaya ya kaskazini ya Waziristan, lilimuuwa mpiganaji mmoja. Shambulio la aina hiyo mwezi Agosti lilimuua kamaanda wa Wataliban wa Pakistan Baitullah Mehsud mwezi.

Lakini Pakistan imelaani hujuma hizo za anga za Marekani, ikisema hazizai matunda yoyote, na badala yake kuwaathiri raia.

Marekani imeitaka Pakistan ichukuwe hatua za ziada kuwaandama wapiganaji wa Taliaban na wale wa Al Qaeda, wakiwemo kutoka nchi jirani ya Afghanistan ambao huvuka mpaka kutafuta maficho ndani ya ardhi ya Pakistan.

Mwandishi:Lazaro Matalange/AFP/DPA

Mhariri:Abdul-Rahman.