1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bashir wa Sudan akubali kikosi cha Umoja wa Mataifa kwa Dafur.

Mohamed Dahman30 Machi 2007

Sudan imekubali kuruhusu kikosi cha Umoja wa Mataifa kujiunga na kikosi cha Umoja wa Afrika katika jimbo lake lenye vurugu la Dafur.Hayo yametangazwa na Saudi Arabia hapo Alhamisi lakini Marekani imeelezea mashaka yake juu ya uamuzi huo wakati ikijiandaa kuiwekea vikwazo vipya Sudan.

https://p.dw.com/p/CHH8
Rais Hassan al Bashir wa Sudan.
Rais Hassan al Bashir wa Sudan.Picha: dpa

Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan kwa muda mrefu amekuwa akipinga uwekaji wa kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika jimbo lake la Dafur lilioko mgharibi mwa Sudan ambapo serikali ya Marekani inasema kumefayika mauaji ya kimbari kupitia hatua ya serikali ya Sudan kuunga mkono makundi ya wanamgambo wanaohama hama.

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Saud al Faisal ameuambia mkutano wa waandishi wa habari katika mkutano wa viongozi wa mataifa ya Kiarabu mjini Riyadh kwamba Sudan hivi sasa imekubali Umoja wa Mataifa itowe msaada kama vile wa kusafirisha watu na vitu kuwasaidia wanajeshi wa Afrika.

Amesema huo ni uvumbuzi ambao haukuwahi kutokea kabla na kwamba wanatumai utapelekea mara moja kufikiwa kwa suluhisho kwa maafa ya kibinaadamu huko Dafur haraka iwezekanavyo.

Afisa mwandamizi wa utawala wa Rais George W. Bush anasema serikali ya Marekani itasubiri kuona iwapo kweli serikali ya Sudan imebadili mkondo wake.Afisa huyo ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters wana mashaka sana kwamba Bashir amekubali jambo kama hilo na kwamba kwanza lazima waone makubaliano hayo halisi.

Kabla ya kutolewa kwa tangazo hilo la serikali ya Saudia maafisa wa serikali ya Marekani kutoka wizara za mambo ya nje, ulinzi,fedha na idara nyenginezo wameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba serikali ya Marekani itazidi kuibana Sudan ambapo hatua mpya dhidi ya nchi hiyo zinatazamiwa kuchukuliwa hivi karibuni.

Hatua hizo ni pamoja na kuweka vikwazo zaidi kwa uhamishaji wa dola wamesema maafisa hao kwa masharti ya kutotajwa majina yao.

Mbali na kuweka vikwazo vya safari na katika benki kwa watu binafsi watatu zaidi akiwemo kiongozi wa waasi serikali ya Marekani inataka kuweka shinikizo zaidi kwa makundi ya waasi yaliogawika gawika.

Marekani pia inakusudia kumshinikiza Bashir kijeshi kwa kusaidia kulijenga upya jeshi la kundi la Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa Sudan SPLA ambalo lilikuwa na vita na serikali ya Sudan ilioko kaskazini mwa nchi hiyo hadi pale walipofikia makubaliano ya amani hapo mwaka 2005.

Ofisa wa wizara ya ulinzi amesema hatua za kijeshi kama vile kupiga marufuku kurusha ndege juu ya anga la Dafur hatua ambayo Uingereza inata ichukuliwe au kuingilia kati kwa nguvu kwa hivi sasa hazizingatiwi.

Wataalamu wanasema takriban watu 200,000 wameuwawa na wengine milioni mbili na nusu wamepotezewa makaazi yao huko Dafur tokea mwaka 2003 wakati waasi walipochukuwa silaha dhidi ya serikali kwa kuishutumu kuwa imepewapuuza.

Serikali ya Sudan inasema ni watu 9,000 waliouwawa na inakanusha kwamba hayo ni mauaji ya kimbari.

Mpango wa Umoja wa Mataifa unataka kupelekwa kwa kikosi kidogo cha kijeshi na kiraia cha Umoja wa Mataifa huko Dafur na kufuatiwa na wanajeshi 2,500 katika awamu ya pili na baadae wanajeshi wengine 10,000 kuunda kikosi cha mchanganyiko na kile cha Umoja wa Afrika.

Tangazo la Saudi Arabia linakuja baada ya Rais Bashir kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, Mkuu wa Umoja wa Waarabu Amr Moussa,Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia na Rais Mwai Kibaki wa Kenya ambaye anaongoza Jumuiya ya Maendeleo ya Mamlaka ya Kiserikali IGAD ya Afrika Mashariki.