1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Biya kugombea urais awamu ya 3

11 Aprili 2008

Rais wa Kamerun amepata idhini ya Bunge kubakia madarakani hadi 2018.

https://p.dw.com/p/DgEM

Bunge la Kamerun limemfungulia mlango kikatiba Rais Paul Biya kubakia madarakani hadi mwaka 2018.Isitoshe, hatafunguliwa mashtaka yoyote atakapon'gatuka madarakani.

Hii ni kwa muujibu wa waziri wa maswali ya katiba Gregoire Owona, alivyoparifu.Alisema kwamba Bunge la Taifa kwa wingi mkubwa limepiga kura kubadili kifungu cha sheria kumwezesha rais Biya mwenye umri wa miaka 75 kugombea tena uchaguzi wa urais hapo 2011.

►◄

Kifungu kingine cha sheria kilichofanyiwa mageuzi na wabunge kinasema "madhambi yaliofanywa na Rais wa Jamhuri hayawezi kukabili mashtaka na rais habebi jukumu lolote baada ya kuondoka madarakani.

Ni wabunge 5 tu waliothubutu kuipinga sheria hiyo na wengine 15 kutoka chama cha upinzani hawakuipigia kura wala kuipinga. Walitoka nje ya Bunge .Wanatoka chama cha Social Democratic Party (SDF).

mmoja kati ya wabunge hao ni JEAN MICHEL NINTCHEU.Alisema:

"Tumesusia kwa sababu tulijua tangu mwanzo kwamba hakuna kitakachobadilika.linapokuja swali la sheria, serikali iliopo madarakani hairuhusu kufanya chochote."

Kura hii Bungeni ilipigwa masaa 24 mapema kuliko ilivyopangwa na tena dakika ya mwisho ili kumsaidia rais Biya kuwasadikisha wabunge 157 kati ya 180 kuungamkono mradi wa kibinafsi uliokua mzizi wa fitina katika maandamano ya mwezi Februari ambamo watu 40 waliuwawa.

Yakichochewa na kupanda kwa ughali wa maisha, maandamano hayo yalizusha machafuko makubwa katika miji mbali mbali ya Kamerun. Mashirika yanayotetea haki za binadamu yalidai idadi hasa ya waliouwawa ni 100 kutokana na mkomoto wa jeshi na polisi.

Mke wa mwimbaji mashuhuri Makossa,bibi Lapiro de Mbanga alietoa nyimbo yake hivi karibuni alioiita "Tumbo la kuharisha la kikatiba", aliliambia jana shirika la habari la kifaransa (AFP) kwamba mumewe amekamatwa siku moja kabla.

Hata kabla machafuko ya kupanda kwa bei za vitu,malalamiko yoyote yale ya kisiasa yalipigwa marufuku katika shina la upinzani - huko Duala.Yalifuatia tangazo la awali la rais Biya juu ya mageuzi ya katiba.

Mwanzoni mwa mwaka huu, rais Paul Biya alitangaza kwamba, anataka kubadili katiba ili kuruhusu watetezi kuweza kugombea awamu ya tatu ya cheo cha rais.Alidai kutoruhusu hivyo, ni kwenda kinyume na msingi halisi wa chaguo la kidemokrasi.

Serikali ya Kamerun imeanzisha hatua kadhaa za kiuchumi kukabiliana na hali mbaya za kimaisha za wananchi.

Waziri wa mawasiliano Jean-Pierre Biyiti, amesema kinyume na vile vyombo vya habari vinavyodai, "Rais Biya hapangi kubaki milele madarakani."