1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush aanza ziara yake ya Mashariki ya Kati

Josephat Charo9 Januari 2008

Rais Bush amelakiwa kwa shangwe nchini Israel

https://p.dw.com/p/CnB3
Rais George W. Bush (kulia) akitembea na rais wa Israel Shimon Peres wakati wa sherehe ya kumkaribisha katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion karibu na mji wa Tel Aviv hii leoPicha: AP

Baraza lote la mawaziri la Israel limemkaribisha rais wa Marekani George W Bush katika ziara yake nchini Israel baada ya kipindi cha muongo mmoja. Rais Bush amefanyiwa gwaride la heshima katika ishara ya kumuunga mkono kiongozi huyo katika zira yake ya Mashariki ya Kati, hali ambayo ni nadra sana kutokea katika ziara zake za kimataifa.

Rais George W Bush wa Marekani akijaribu kuzishinikiza Israel na Palestina ziyaendeleza mazungumzo ya kutafuta amani, amesema leo kwamba anazuru Israel akiwa na matumaini makubwa ya makubaliano ya amani kufikiwa kabla kumaliza awamu yake madarakani.

Rais Bush amekutana na rais wa Israel, Shimon Peres, mjini Jerusalem. Msafara wa rais Bush umewasili katika makao makuu ya rais Peres chini ya ulinzi mkali muda wa saa tatu baada ya ndege iliyombeba kutua katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion nje ya mji wa Tel Aviv.

Mlolongo wa watoto waliobeba bendera za Israel na Marekani, ulimkaribisha rais huyo wa Marekani na kumuimbia wimbo maarufu kwa lugha ya kiebrania uitwao Shalom Aleikhem, yaani amani iwe nawe.

Rais Bush alijumuika na watoto hao waliokuwa wamevalia shati nyeupe kabla kuingia ndani ya ikulu ya rais Peres ambamo msichana mdogo amewaimbia wimbo uitwao ´Somewhere Over the Rainbow´ na kuwapa viongozi hao wawili maua ya waridi.

´Ni muhimu dunia iendelee kupambana na ugaidi,´ amesema rais Bush wakati alipoanza ziara yake rasmi nchini Israel ambako ameanza mazungumzo na rais wa nchi hiyo, Shimon Peres. Rais Perez amesema, ´Bwana rais tunakukaribisha hapa kama rafiki mkubwa. Tunakuheshimu kama kiongozi wa taifa lenye heshima kubwa ambalo baada ya kupata uhuru wake, halikuchoka kuyapa mataifa mengine uhuru huu.´

Rais Peres amesema wakati huu ni muhimu sana kwa juhudi za kukabiliana na ugaidi na amemshukuru rais Bush kwa kuisaidia Israel bila kuyumbayumba.

´Tunazingatia wosia wako kutopuuza kitisho cha Iran. Iran haipaswi kupuuza ukakamavu wetu wa kujilinda.´

Rais Bush amesema hii ni nafasi mpya kwa eneo la Mashariki ya Kati kufikia amani.

´Ni nafasi mpya kwa amani hapa katika nchi takatifu na kwa uhuru katika eneo zima la Mashariki ya Kati. Nasubiri kwaa hamu kukutana na rais Peres na waziri mkuu Olmert. Tutajadili juu ya ari yetu ya ulinzi, uhuru na amani.´

Mamia ya Wapalestina wamefanya maandamano mjini Gaza kupinga ziara ya rais Bush. Wafuasi wa vitengo mbalimbali vya chama cha Palestine Liberation Movement, PLO, wameandamana katika barabara za mjini Gaza wakipiga kelele wakimlaani rais Bush na kumtaka aache upendeleo. Baadhi yao walibeba mabango yaliyokuwa na maneno yaliyosema rais Bush hakaribishwi katika maeneo ya Wapalestina.

Katika mji wa Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, kundi ambalo zamani lilikuwa halijulikani linalojiita Army of the Nation, yaani jeshi la taifa, limeapa kumuua rais Bush pamoja na Wamarekani wote likimueleza kiongozi huyo kuwa mhalifu.

Kundi lenye siasa kali la Islamic Jihad lilifanya maandamano mjini Gaza jana usiku na kundi la Islamic Hamas kwa upande wake linapanga kufanya maandamano makubwa mjini humo hapo kesho wakati rais Bush atakapokuwa akikutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas.