1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush aita Iran tishio la usalama duniani

14 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CpAZ

ABU DHABI

Rais George W. Bush wa Marekani ametowa wito kwa washirika wake katika Ghuba ya Uajemi kukabiliana na Iran.

Katika hotuba yake mjini Abu Dhabi Umoja wa Falme za Kiarabu ameishutumu Iran moja kwa moja kwa kuunga mkono ugaidi.

Bush anasema Iran leo hii ni mdhamini mkuu wa ugaidi duniani na inatuma mamilioni ya dola kwa Waislamu wa itikadi kali duniani kote wakati watu wake wakikabiliwa na ukandamizaji na shida huko nyumbani kwa hiyo Marekani inaimarisha majukumu yake ya usalama ya muda mrefu na marafiki zake wa Ghuba na kutafuta uungaji mkono wa marafiki duniani kote kukabiliana na hatari hiyo kabla ya kuchelewa kuchukua hatua.

Katika hotuba yake hiyo Bush pia amesema kwamba Iran inadhoofisha utulivu nchini Lebanon kwa kuunga mkono kundi la itikadi kali la Hizbollah pamoja na kuunga mkono kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas na waasi wa Kishia nchini Iraq.

Bush leo anaelekea Saudi Arabia ambapo atakuwepo kwa siku mbili baada ya kuzitembelea Israel na Ukingo wa Magharibi, Kuwait Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu .

Atakamilisha ziara yake ya Mashariki ya Kati kwa kuitembelea Misri kabla ya kurudi Marekani hapo Jumaatano.