1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush aonya juu ya mapigano na umwagaji damu mkubwa Iraq

Mohamed Dahman25 Mei 2007

Rais George W. Bush wa Marekani ameonya juu ya kutokea kwa mapigano makubwa na umwagaji damu nchini Iraq ambapo amesema miezi michache inayokuja itakuwa ni wakati mgumu kwa mkakati mpya wa Marekani kwa Iraq.

https://p.dw.com/p/CB3x
Rais George W. Bush wa Marekani.
Rais George W. Bush wa Marekani.Picha: AP

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani hapo jana Rais Bush amesema anategemea kuzuka kwa mapigano makubwa baada ya kuongezwa kwa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ifikapo kati kati ya mwezi wa Juni.

Onyo hilo la Bush limekuja wakati bunge la Marekani likiidhinisha muswada wa kugharamia vita vya Iraq na Afghanistan.

Kipindi hiki cha majira ya kiangazi kitakuwa kigumu kwa mkakati mpya Bush amesema hayo hapo jana katika mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani ulionyeshwa moja kwa moja na vituo vya televisheni vya Marekani.

Amesema wanategemea kuzuka kwa mapigano makubwa katika wiki na miezi inayokuja na kutabiri umwagaji damu zaidi wakati mkakati wake wa kuongeza zaidi ya wanajeshi 30,000 nchini Iraq ukiwa unafikia kileleni.

Amesema wakati vikosi hivyo vilivyoimarishwa vikitekeleza kazi zao maadui wa Iraq ilio huru wakiwemo Al Qaeda na wanamgambo wasio halali wataendelea kuripua mabomu na kuuwa katika jaribio la kuwazuwiya. Amesema wanatarajia maafa zaidi ya Wamarekani na Wairaq na hiyo kutaka wanajeshi wao wapatiwe fedha na rasilmali wanazohitaji kuibuka washindi.

Generali mkuu wa Marekani nchini Iraq David Petraeus anatazamiwa kurepoti hapo mwezi wa Septemba juu ya maendeleo ya mkakati huo na Bush ametabiri kwamba maadui wa Marekani nchini Iraq watafanya kila wawezalo katika kipindi hicho kushawishi mjadala juu ya vita vya Iraq nchini Marekani.

Onyo la Bush limekuja wakati bunge la Marekani likijiandaa kupiga kura muswada wa kugharamia vita vya Iraq na Afghanistan wa dola bilioni 120 kuchukuwa nafasi ya muswada wa awali ambao aliupinga kwa kura ya turufu mapema mwezi huu kutokana na kuweka tarehe ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq.

Baraza la Wawakilishi limeuidhinisha muswada huo kwa kura 280 dhidi ya 142 kugharamia vita vya Iraq hadi mwezi wa Septemba mwaka huu baada ya wabunge wa chama cha Demokrat kukubali shingo upande madai ya Bush ya kufuta vipengele vinavyotaja tarehe ya kuondowa wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq wakati baraza la Senate limeuidhinisha muswada huo kwa kura 80 dhidi ya 14.

Rais Bush amesema muswada huo wa sheria unaonyesha muafaka na amewataka viongozi wa Iraq kulipa kujitolea muhanga kwa Marekani kwa kufanya maendeleo ya kisiasa.

Licha ya tahadhari zake kwamba kujitowa na mapema kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq kutakuwa ni maafa amesema hatokuwa na chaguo isipokuwa kuamuru kuondolewa kwa vikosi hivyo iwapo serikali ya Iraq itadai hivyo.

Bush ameongeza kusema kwamba kushindwa nchini Iraq kutasababisha vizazi kwa vizazi kuteseka na kundi la Al Qaeda litazidi kuimarika.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates naye pia ameonya dhidi ya kuwa na matarajio makubwa mno ya maendeleo ya haraka nchini Iraq kwamba hawawezi kubadili hali ya nchi hiyo kwa kucha moja.