1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush azindua mpango wa kupambana na malaria

18 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D9KP

Rais George W Bush wa Marekani leo amezindua mpango wa mpya wa kupambana na ugonjwa wa malaria mjini Arusha nchini Tanzania.

Mpango huo unalenga kuwapa mamilioni ya watoto watanzania vyandarua vya kuwalinda kutokana na mbu wanaosababisha ugonjwa hatari wa malaria.

Rais Bush wa Marekani ameutembelea mji wa Arusha hii leo akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake nchini Tanzania.

Baada ya kuitembelea hospitali ya wilaya ya Meru mjini Arusha, rais Bush amesema vyandarua vya kuzuia mbu ni mojawapo ya teknolojia rahisi lakini inayofaa kuleta matokeo yanayotarajiwa.

Rais Bush pia amezungumzia kuhusu msaada wa Marekani kwa fuko la fedha la kimataifa la kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria, akigusia kampeni za kunyunyiza dawa za kuua wadudu, kuwatibu watoto na akina mama wajawazito na kusambaza vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa ya kuua mbu.

Tanzania ni kituo cha pili cha ziara ya siku sita ya rais Bush barani Afrika iliyoanza nchini Benin Jumamosi iliyopita.

Rais Bush atazitembelea pia Rwanda, Ghana na Liberia kabla kurejea mjini Washington.