1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush ziarani Korea ya kusini

Hamidou, Oumilkher5 Agosti 2008

Rais wa Marekani anafanya ziara ya wiki moja barani Asia,ziara itakayomfikisha pia Bangkok na Beijing

https://p.dw.com/p/EqzG
Maandamano ya wakorea dhidi ya ziara ya rais BushPicha: AP



Rais George W. Bush wa Marekani amewasili Korea ya kusini hii leo,kituo cha kwanza cha ziara ya wiki moja barani Asia,itakayomfikisha pia Thailand,kabla ya kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa michezo ya Olympic mjini Beijing.



Ndege ya rais huyo wa Marekani Air Force One ,imetuwa katika uwanja wa ndege wa kijeshi kusini mwa mji mkuu wa Korea ya Kusini-Seoul.


Baadae hii leo rais Bush aliyefuatana na mkewe Laura,amepangiwa kukutana na kiongozi mwenzake Lee MYUNG-Bak,na baadae kuwahutubia wanajeshi wa Marekani katika kituo cha Yongsan mjini Seoul kabla ya kuondoka kesho jioni kuelekea Bangkok nchini Thailand.


Nchini Korea ya kusini,mshirika wa karibu sana wa Washington barani Asia,rais George W. Bush anapanga kulizusha suala la mradi wa kinuklea wa Korea ya kaskazini na kusahihisha mkataba wa biashara huru unaozusha mabishano hasa baada ya kuanza upya kuingizwa nchini Korea ya kusini nyama ya ngombe ya Marekani.



Zaidi ya askari polisi 20.000 na maelfu kadhaa ya wanajeshi wametawanywa majiani kuepusha pasitokee machafuko wakati wa ziara ya rais huyo wa Marekani.


Makundi ya wakorea ya kusini wamekusanyika na kuasha mishumaa,kulalamika dhidi ya kuanza upya kuingizwa nchini mwao nyama ya ngombe ya Marekani.Wanahofia isiwe nyama hiyo inatokana na ngombe walioshikwa na maradhi ya kichaa cha ng'ombe.


Maandamano kadhaa yaliitishwa April iliyopita pale serikali ya Korea kusini iliporuhusu upya nyama ya ngombe iliyopigwa marufuku tangu mwaka 2003 iaigiziwe upya kutoka Marekani.


Maandamano hayo yalisita lakini baada ya Washington kuhaakikisha "hakuna nyama ya kichaa cha ngombe itakayoingia Korea ya kusini."


Kuna sababu nyengine pia zinazowakera baadhi ya wakorea ya kusini.Bibi Mmoja anasema:



"Tunaandamana ili wanajeshi wa Marekani waihame Korea."


Marekani ina wanajeshi kama 28 elfu na mia tano nchini Korea ya kusini.Wananchi wengi wanawaangalia wanajeshi hao kama pingamizi ya kupatikana suluhu kati ya Korea mbili.


Wimbi la malalamiko lilikua chanzo cha kuakhirishwa ziara ya rais Bush iliyokua kimsingi ifanyike mwezi uliopita nchini humo.


Sambamba na wimbi la malalamiko,wapiganaji 30 elfu wa zamani wa vita vya Korea kati ya mwaka 1950 hadi 1953 na wahafidhina wa kikristo wamekusanyika kushadidia umuhimu wa uhusiano kati ya Seoul na Washington.


Upande wa kidiplomasia,suala la mradi wa kinuklea wa Korea ya kaskazini linatazamiwa kugubika mazungumzo kati ya rais Bush na mwenyeji wake Lee Myung-Bak.


Ziara ya rais Bush inafanyika siku chache kabla ya muda uliopangwa wa Korea ya kaskazini kukubali itifaki ya kuchunguza harakati za mitambo yake ya kinuklea.Muda huo utakamilika Agosti 11 ijayo.