1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Gbagbo kufanya ziara ya kihistoria katika mji wa Bouake makao makuu ya zamani ya waasi.

Mohamed Dahman29 Julai 2007

Rais Laurent Gbagbo leo hii atakuwepo katika mji wa Bouake makao makuu ya kundi la zamani la waasi la New Forces FN kwa ajili ya sherehe za kusalimisha silaha za waasi.Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Gbagbo kuzuru mji huo tokea uasi wa mwaka 2002 uliokusudia kumpinduwa kuigawa Ivory Coast pande mbili.

https://p.dw.com/p/CHAO
Rais Laurent Gbagbo wa Ivory Coast.
Rais Laurent Gbagbo wa Ivory Coast.Picha: AP

Sherehe hizo zinatazamiwa kuhudhuriwa na marais kadhaa wa Afrika kuupa nguvu mchakato wa amani wa nchi hiyo ya Afrika magharibi.

Ilikuwa ni kutokea Bouake kwamba nusu ya pili ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi ilikuwa ikidhibitiwa na waasi kwa takriban miaka mitano.

Gbagbo atakuwa mgeni wa heshima katika sherehe kubwa za kusalimisha silaha na usuluhishi katika hatua muhimu ya kuelekea amani ya kudumu nchini humo ambayo imeiunganisha tena nchi hiyo.

Rundo la silaha litatiwa moto kuashiria kuanza rasmi kwa usalimishaji silaha katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo.

Zikipewa jina la Moto wa Amani tukio hilo pia ni sherehe za usuluhishi ambao umekuwepo kufuatia makubaliano ya amani ya karibuni yaliofikiwa chini ya upatanishi wa nchi jirani ya Burkina Faso kati ya Gbagbo na kundi la waasi la FN.

Makubaliano hayo mapya yameweza kupiga hatua kubwa zaidi kuliko majaribio ya usuluhishi yaliopita chini ya usimamizi wa mkoloni wa zamani wa nchi hiyo Ufaransa,Umoja wa Mataifa,Umoja wa Afrika halikadhalika jumuiya ya Afrika magharibi.

Hata hivyo kuna vikwazo kadhaa vinavyozorotesha utekelezaji wa makubaliano hayo.Vikwazo hivyo ni pamoja na kulifanyia mageuzi jeshi na daftari la wapiga kura kabla ya uchaguzi wa nchi hiyo mambo ambayo yalikuwa yaanze kutekelezwa hapo mwezi wa April.

Sherehe hizo za Bouake ambazo zimeahirishwa mara kadhaa zinafanyika kukiwa na hali ya wasi wasi fulani na hofu ya kuzuka kwa machafuko.

Kufuatia jaribio la kuuwawa kwa Soro vikosi vya serikali vimewekwa katika hali kubwa ya tahadhari kutokana na hofu ya kuzuka kwa mashambulizi mapya.

Ilikuwa ni katika mji wa Bouake hapo tarehe 29 mwezi wa Juni kwamba ndege iliokuwa imemchukuwa Guillaume Soro kiongozi wa zamani wa waasi wa kundi la New Forces FN iliposhambuliwa wakati ilipokuwa inatua.Soro ambaye tokea mwezi wa April amekuwa waziri mkuu alinusurika kwenye shambulio hilo lakini wasaidizi wake wanne waliuwawa.

Soro kwa haraka alijaribu kuzima tetesi juu ya nani aliehusika na shambulio hilo na kutowa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kimataifa utakaoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Hivi karibuni amekaririwa akisema kwamba watahakikisha kwamba kile watu watakachoikumbukia Bouake ni amani na sio vita.

Kambi ya upande wa Gbagbo inapanga kuwasafirisha maelfu ya wafuasi kwenda Bouake kuhudhuria sherehe hizo ambako kunaonekana pia ni kujiamarisha kimadaraka kwa rais huyo mwenye msimamo mkali.

Gbagbo ameitangaza siku ya leo kuwa ni ya mapumziko na amewaalika marais kadhaa kuhudhuria sherehe hizo ambao ni Blaise Compaore wa Burkina Faso,Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na kiongozi wa Ghana ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika John Kufour.Wengine ni Abdoulaye Wade wa Senegal.Faure Yassingbe wa Togo,Amadou Toumani Tuore wa Mali na Yayi Boni wa Benin.

Zaidi ya wanajeshi 1,000 wa serikali na waasi wa zamani wataungana pamoja kuwapa ulinzi marais hao na kusimama kwao bega kwa bega itakuwa ni ishara ya nguvu ya usuluhishi kwamba vita vimekwisha kweli nchini Ivory Coast.