1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Hollande katika kashfa ya ngono

Admin.WagnerD15 Januari 2014

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amekiri kuwa anapitia wakati mgumu yeye na mpenzi wake, baada ya jarida moja kuripoti kwamba kiongozi huyo alikuwa na uhusiano wa siri na muingizaji filamu mmoja wa kike.

https://p.dw.com/p/1AqkX
Nakala za jarida la Closer lilipoibua kashfa ya Hollande.
Nakala za jarida la Closer lilipoibua kashfa ya Hollande.Picha: picture-alliance/dpa

Lakini rais huyo msoshalisti ambaye umaarufu wake uko chini kabisa kuliko rais yeyote aliyewahi kuiongoza Ufaransa, alijaribu kukwepa kuzungumzia kashfa hiyo wakati wa mkutano wake wa kila mwaka na waandishi wa habari, na badala yake alijikita katika mpango wake wa kufufua uchumi wa Ufaransa.

Mpenzi wa Hollande, mwandishi wa habari Valerie Trierweiler amelazwa hospitalini tangu siku ya Ijumaa, baada ya jarida la udaku liitwalo Closer kuchapisha picha ambazo lilisema zinathibitisha kuwa Hollande alikuwa na uhusiano na muingizaji Julie Gayet kwenye kona ya karibu na kasri ya rais ya Elysee.

Rais Hollande akijibu maswali ya waandishi katika mkutano wake wa mwaka.
Rais Hollande akijibu maswali ya waandishi katika mkutano wake wa mwaka.Picha: Reuters

Akiri kuwa katika wakati mgumu
Alipoulizwa swali la moja kwa moja iwapo mpenzi wake Trierweiler alikuwa bado ndiye rasmi kwa rais wa Ufaransa, Hollande alisema mkutano huo haukuwa mahala pa kuzungumzia suala hilo.

"Naelewa swali lako, na nina uhakika utaelewa jibu langu pia. Kila moja katika maisha yao binafsi wanaweza kupitia wakati mgumu, na hilo ndiyo linalotokea kwangu sasa hivi. Lakini nina kanuni moja, masuala binafsi yanashughulikiwa kibinafsi. Huu sio wakati wake na hapa siyo mahala pake, kwa hivyo sitojibu swali lako kuhusu maisha yangu binafsi," alisema Hollande.

Hollande hakukanusha wala kuthibitisha ripoti za jarida la Closer, lakini tangazo lake la jana Jumanne kuhusu hatua za kiuchumi zenye lengo la kuhamasisha uundaji wa nafasi zaidi za ajira liligubikwa na sakata hilo. Hollande alisema angejibu swali kuhusu mpenzi wake kabla ya zaira yake ya Februari 11 mjini Washington, ziara ambayo kwa kawaida inapaswa kumhusisha Trierweiler.

Ripoti ya jarida la Closer ilionyesha picha za mwanaume iliyomtambua kuwa ni Hollande akiwa amevaa kofi ya kinga kwenye pikipiki akiendeshwa nyuma ya pikipiki aina ya scooter kuelekea katika hoteli iliyopo karibu na Elysee kwa miadi na hawara yake Gayet. Hollande ambaye umaarufu wake uko katika kiwango cha chini kabisaa, anaonekana kuepuka madhara makubwa ya kisiasa kutokana na sakata hilo.

Rais Hollande akiwa na mpenzi wake Valerie Trierweiler.
Rais Hollande akiwa na mpenzi wake Valerie Trierweiler.Picha: picture-alliance/dpa

"Ni maisha yake binafsi"
Uchunguzi wa maoni umeonyesha kuwa zaidi wa watatu kati ya wapiga kura wanne wanaamini maisha ya mapenzi ya Hollande ni mambo yake binafsi, na utafiti mwingine ulionyesha kuongezeka kidogo kwa uungwaji mkono wa kiongozi huyo.

Hollande alitumia dakika 45 za ufunguzi wa mkutano wake kwa kubainisha sera mpya ya kiuchumi inayonuwia kuchochea ukuaji na kuunda nafasi za ajira. Kipaumbele cha mpango wake huo ni makato ya kiasi cha euro bilioni 30 katika kodi zinazolipwa na waajiri kutokana na mishahara ya waajiriwa wao ifikapo mwaka 2017, kwa kufuta kile kinachoitwa michango ya familia inayolipwa na makampuni kwa wafanyakazi wa kujitegemea. Lakini alisema kuyapunguzia kodi makampuni hakutosawazishwa kwa kuzitoza kodi zaidi familia.

Mwandishi:Iddi Ismail Ssessanga/afpe,ape,dpae
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman