1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Hugo Chaves wa Venezuela ataka katiba ya nchi ibadilishwe

Siraj Kalyango30 Novemba 2007

Wapinzani wasema eti hatua yake inatishia demokrasia.

https://p.dw.com/p/CVDc
Wanafunzi waandamana dhidi ya serikali mjini CaracasPicha: AP

Kiongozi wa Venezuela, Hugo Chaves, anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwanyamazisha wanaoshuku uongozi wake.Ameitisha kura ya maoni kuhusu kuibadilisha katiba.Kura hii ikifaulu itampa uwezo zaidi kuliko alionao sasa.

Hugo Chaves,ameiongoza nchi hiyo kwa miaka minane iliopita.Na anataka kuitawala zaidi,lakini katiba ya nchi hairuhusu hilo,ila ikiwa wananchi wataamua hivyo ndoto yake inaweza ikatimia.Na anaamini kuwa ni kipenzi cha walala hoi ambo ni wengi nchini humo.

Kutokana hilo,anajaribu bahati yake kwa kuomba wananchi ruhusa.

Ombi liko katika kura ya maoni ya kuibadilisha katiba ambayo inafanyika jumapili.

Lakini hatua yake hii inawakanganya sio tu maadui zake lakini pia na wafuasi wake.

Wapinzani wake wakiongozwa na wanafunzi wa chuo kikuu, walipambana na askari wa kutuliza ghasia hiyo Ijumaa walipoandamana katika barabara za mjini Caracas,mji mkuu wa Venezuela.Polisi imetawanya maandamano hayo kwa kutumia risasi za mipira pamoja na kutumia gesi zinazosababisha makamasi.

Waandamanaji wanapinga hatua zake ambazo zinaonekana kama kutaka kuibadilisha nchi hiyo kuwa ya kisoshalisti jambo ambalo wengi wanapinga.

Miongoni mwa mabadiliko anayotaka yafanyiwe katiba katika kura hii ya maoni ni: kutaka kukubaliwa kugombea uongozi bila kikomo; kutangaza hali ya hatari;kuvikabili vyombo vya habari na kujizatiti zaidi kwa kukubaliwa kuwateua maafisa katika ngazi za mikoa.

Anaonekana anataka kuingiza mawazo yake ya kimapinduzi kwa kuitangaza nchi hiyo kuwa ya kisoshalisti.Anataka kutaifishwa kwa mali za kibnafsi,mithili ya Cuba chini ya Fidel Castro.

Chaves anadai kuwa mageuzi hayo si kwa manufaa yake mwenyewe bali kwa wananchi wa kawaida.

Lakini mageuzi hayo yatakumbana na upinzani hata kutoka kwa mshirika wake wa zamani Raul Baduel aliekuwa waziri wa Ulinzi.Baduel ameziita hatua za sasa za Chaves kama tisho kwa demokrasia.Yeye rais amewaita wapinzani wa mpango huo kama wasaliti.

Jamii ya kimataifa imemulika macho yake kwa kura hiyo.Hii ni kwa sababu,Venezuela ni mwanachama wa kundi la nchi ambazo zinazalisha mafuta kwa wingi duania OPEC.Halafu ni mmojawapo wa nchi zinazoiuzia Marekani mafuta.

Kutokana na kuwa ana mwelekeo wa kijamaa, anapingwa na utawala wa Washington.Maendeleo pamoja na fikra za Chaves zimekuwa zikiipa Marerkani tumbo-joto na inafuatilia kwa makini kura ya jumapili.

Chaves anaituhumu Marekani kwa kuunga mkono njama za majaribio ya mapinduzi yaliyoshindwa dhidi yake mwaka wa 2002.

Sio tu Marekani inayomuombea dua mbaya Chaves, lakini pia na majirani zake.Rais Alvaro Uribe wa Colombia amekuwa akitupiana maneno makali na cheo somo wake wa Venezuela, na hivyo kumfuta kama mpatanishi kati ya utawala wa Bogota na waasi wa mrengo wa kushoto wa Colombia wa FARC.

Chaves anaonekana kama mtu anaetetea maslahi ya wanyonge katika Amerika ya Kusini kwa upande mmoja huku upande wa pili anamchukulia kama asieitaka Marekani.Eti anatumia mafuta ya nchi yake kama silaha ya kisiasa na mwenye domo kaya.

Chaves mwenye umri wa miaka 53, ni mzungumzaji mzuri,ambae amekuwa akishangiliwa kila akitoa hutuba kwa wafuasia wake. Hata hivyo wakati mwingine amekuwa akitoa kauli za utata ambazo upande mmoja unazichukulia kama za kiuchokozi.

Haijulikani ikiwa mbinu zake pamoja na umaarufu wake utamsaidia kupata kile anachotaka katika kura ya maoni ya hapo jumapili.

Kwa vyovyote vile ile sifa ya kuwa yeye ndie mwanasiasa asietetereka katika bara la Amerika ya kusini baado inaiendeleza.