1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Joachim Gauck ziarani Amerika Kusini

Admin.WagnerD9 Mei 2013

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck leo (09.05.2013) anaanza ziara ya siku tisa katika bara la Amerika Kusini, ambayo itampeleka kwanza Colombia na baadae Brazil, mshirika muhimu zaidi wa Ujerumani Amerika ya Kusini.

https://p.dw.com/p/18Upl
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck baada ya kuwasili mjini Bogota, Colombia.
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck baada ya kuwasili mjini Bogota, Colombia.Picha: picture-alliance/dpa

Akiwa nchini Brazil, ambayo ndiyo taifa la sita kwa uchumi mkubwa duniani, Gauck anatarajiwa kujikita katika masuala ya kiuchumi, na nchini Colombia atazungumzia haja ya maridhiano ya kitaifa. Serikali ya Colombia kwa sasa inashiriki mazungumzo na kundi la waasi wa "Revolutionery Armed Forces of Colombia" FARC, mchakato ambao kwa mara ya kwanza umeonyesha matumaini ya kufanikiwa. Mgororo wa nchi hiyo uliodumu kwa nusu karne sasa, umegharimu maisha ya watu karibu laki mbili, na kusababisha wengine milioni 4 kuyakimbia makaazi yao.

Rais wa Colombia, Juan Manuel Santos.
Rais wa Colombia, Juan Manuel Santos.Picha: Reuters

Gauck ambae ni mchungaji wa zamani wa kilutheri na mwanaharakati wa kupinga ukomunisti kutoka Ujerumani ya Mashariki, ana uzoefu mkubwa katika mchakato wa ushirikishwaji na anatarajiwa kuzungumzia suala hilo mara nyingi wakati wa ziara yake. Ujerumani inajiona kama mshirika katika mdahalo wa Colombia, na imekuwa ikielekeza msaada wake kwa uendelezaji wa mchakato wa amani. Ingawa hali ya haki za binaadamu nchini humo haiwezi kuchukuliwa kama isiyo na matatizo, serikali ya rais wa Colombia Juan Manuel Santos inachukuliwa kuwa katika njia sahihi kwa mujibu wa ofisi ya rais wa Ujerumani.

Maridhiano miongoni mwa jamii ya Wacolombia ni sharti la kupatikana kwa mafanikio ya kiuchumi. Serikali ya Ujerumani imeikubali Colombia kuwa miongoni mwa shabaha zake za masoko, na nchi hiyo ndiyo mshirika mkuu wa Kibishara wa Colombia katika bara la Ulaya, na kimataifa, ujerumani ni nchi ya nne nyuma ya Marekani, China na Mexico.

Uchumi kuzungumzwa Brazil

Rais Gauck ataizuru Brazil siku ya Jumapili, ambapo masuala ya kiuchumi ndiyo yatakuwa kwenye ajenda yake. Ziara yake mjini Sao Paulo itaashiria kuanza kwa mwaka wa Ujerumani katika taifa hilo la Amerika Kusini, ambao mtangulizi wa Gauck Chritian Wulff alikubaliana na Rais wa Brazil Dilma Rousseff kuuanzisha mei 2011.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameizuru Brazil mara moja tu katika uongozi wake, mwaka 2008. Mwaka uliyopita, alifuta ushiriki wake katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu, maarufu kama Rio+20, jambo lililowasikitisha Wabrazil. Jumuiya ya wafanyabiashra wa Ujerumani nchini Brazil wangependa kumuona Merkel tena, kwa sababu nchi hiyo ndiyo mshirika imara zaidi wa kiuchumi wa Ujerumani katika Amerika ya Kusini, na Gauck anatizamiwa kusafisha njia kwa ajili ya ziara hiyo.

Rais wa Brazil, Dilma Rousseff.
Rais wa Brazil, Dilma Rousseff.Picha: Reuters

Gauck anaongoza ujumbe mkubwa wa kiuchumi, unaojumlisha wataalamu wa mazingira na teknolojia ya dawa, uhandisi, usafiri wa anga na usafirishaji, pamoja na wawakilishi wa sekta ya ujenzi na usanifu majengo. Wafanyabiashara wa Ujerumani wanatumaini kushiriki katika miradi ya ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mashindano ya kombe la dunia mwaka 2014, na michezo ya olimpiki mwaka 2016 na pia katika upanuzi wa bandari za nchi hiyo.

Kuna karibu makampuni 800 ya Ujerumani yanayoendesha shughuli zake katika mji wa Sao Paulo peke yake. Mji huo unaoshikilia uchumi wa Brazil ndiyo unaochukuliwa kuwa na shughuli nyingi za viwanda vya Kijerumani nje ya Ujerumani. Lakini uchumi wa nchi hiyo ulipungua kasi na kufikia kiwango cha ukuaji cha asilimia 0.9 tu mwaka uliyopita, huku mfumuko wa bei ukiwa asilimia 5.8, na unatarajiwa kuendelea kuwa katika kiwango hicho mwaka huu.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae
Mhariri: Saum Yusuf.