1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Jonathan aapa kuwaadhibu wafadhili wa Boko Haram

23 Januari 2012

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria amesema watu wanaoshukiwa kuhusika na mashambulizi ya wiki iliyopita mjini Kano, ambayo yameua zaidi ya watu 160 wameanza kukamatwa huku akiapa tena kuliangamiza kundi la Boko Haram.

https://p.dw.com/p/13oEV
Rais Jonathan Goodluck wa Nigeria.
Rais Jonathan Goodluck wa Nigeria.Picha: AP

Rais Jonathan aliyazungumza hayo baada ya kulitembelea jimbo la kaskazini la Kano kuzifariji familia zilizoathirika vibaya na mashambulizi ya hapo Ijumaa, ambapo miripuko na mapigano ya risasi baada ya sala ya Ijumaa yaliutikisa mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Nigeria.

"Baadhi ya watu wameshakamatwa. Wengine walikuwa katika harakati hizo. Wengine walikuwa ni wauaji wa kujitoa muhanga." Amesema Rais Jonathan.

Rais Jonathan aliwatembelea majeruhi walioko hospitali na pia mabaki ya majengo yaliyovurugwa vibaya na mashambulizi hayo, likiwemo la makao makuu ya polisi ya Kano. Hadi sasa watu 166 wanaripotiwa kufariki dunia, miongoni mwao wakiwa wataalamu watatu kutoka India, ambao walijikuta wakiwa katikati ya urushianaji risasi.

Kwa mujibu wa Rais Jonathan, mashambulizi hayo ya kigaidi yamefanywa na Boko Haram na kwamba kundi hilo linafadhaliwa na vyanzo mbalimbali.

"Lazima kutakuwa na watu wanaowafadhili, kwani magaidi kote duniani huwa wana vyanzo vyao vya mapato. Tunawatafuta katika maeneo yote ili kuhakikisha kuwa hao wanaoitwa Boko Haram, wale wanaowaunga mkono na wale wanaowafadhili, wote wanaadhibiwa." Amesema Rais Jonathan.

Watu wakikimbia baada ya mashambulizi mjini Kano.
Watu wakikimbia baada ya mashambulizi mjini Kano.Picha: Reuters

Naye mkuu wa Jumuiya ya Wakristo wa Nigeria katika jimbo la Kano, Askofu Ransom Bello, amesema kwamba haamini ikiwa Boko Haram inawakilisha mtazamo wa Waislamu nchini humo.

"Mashambulizi haya hayanitishi mimi binafsi wala jamii ya Kikristo. Yamefanywa na Boko Haram na sio na jamii ya Waislamu wa Nigeria. Hapa kwenye jimbo la Kano tunafanya kazi pamoja sote, Waislamu na Wakristo. Kwa hivyo hatuamini kuwa mashambulizi haya yatafanya kazi. Hatuhami, tunabakia hapa hapa." Amesema Askofu Bello.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Boko Haram ni kundi linaloishi kama kivuli likiaminika tu kuwa linakusanya makundi mengine mengi ndani yake yenye malengo yanayotafautiana, baadhi yakiwa ya kisiasa na mengine ya misimamo mikali ya kidini.

Ziara hiyo fupi ya Rais Jonathan mjini Kano ilitandwa na kiwango kikubwa cha vikosi vya usalama, vifaru vya kijeshi na magari ya doria. Alifanya mazungumzo na kiongozi wa Waislamu wa eneo hilo, Amir Ado Bayero, na kumuahidi kwamba angelifanya kila awezalo kuhakikisha usalama, akirejea kauli yake ya baada ya mashambulizi ya Krismasi, kuwa "mashambulizi dhdi ya Mnigeria mmoja, ni sawa na mashambulizi dhidi ya taifa zima."

Wafanyakazi wa huduma za uokozi katika moja ya maeneo ambayo kulfanyika mashambulizi mjini Kano.
Wafanyakazi wa huduma za uokozi katika moja ya maeneo ambayo kulfanyika mashambulizi mjini Kano.Picha: Reuters

Ziara hii imefanyika masaa machache tu baada ya mashambulizi mengine kufanywa kwenye mji wa Tafawa Balewa, ambao uko kwenye jimbo jirani la Bauchi. Katika mashambulizi hayo ya alfajiri, watu wenye silaha waliwauwa watu 10, huku pia mabomu yakiripotiwa kurushwa kwenye makanisa katika mji mkuu wa jimbo la Bauchi. Polisi mjini Kano, imesema kwamba imefanikiwa kulitegua bomu moja katika gari.

Kwa ujumla hali mjini Kano ni shwari ingawa wasiwasi umetanda katika mitaa ya mji huo. Polisi imeweka vizuizi vya barabarani baada ya kulegeza amri yake ya kutotoka nje iliyokuwa imetangazwa hapo Ijumaa.

Rais Jonathan alikuwa ametangaza hali ya hatari katika sehemu kadhaa nchini Nigeria, kufuatia mashambulizi ya Krismasi, lakini amri hiyo haikujumuisha mji wa Kano, ambao hadi hapo ulikuwa bado salama.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf