1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Jonathan kugombea uchaguzi mwakani

11 Novemba 2014

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, leo ametangaza rasmi nia yake ya kuwania kiti cha urais kwa muhula mwingine wa pili, katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Februari mwaka ujao wa 2015.

https://p.dw.com/p/1DlSc
Rais Goodluck Jonathan
Rais Goodluck JonathanPicha: imago/Wolf P. Prange

Rais Goodluck Jonathan ametangaza rasmi nia hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo mjini Abuja. Amesema atagombea kiti cha urais kupitia tiketi ya chama tawala cha Peoples Democratic Party-PDP. Akizungumza na wafuasi wa chama cha PDP, kiongozi huyo wa Nigeria alisema, namnukuu: ''Mimi Goodluck Ebele Azikiwe Jonathan, nimekubali kugombea katika uchaguzi kwa tiketi ya chama cha PDP,'' mwisho wa kumnukuu.

Rais Jonathan mwenye umri wa miaka 56, amesema amechukua uamuzi huo baada ya kutafuta hekima na msaada wa Mungu na kupata ushauri wa familia yake. Magavana wa majimbo wa chama tawala pamoja na kamati kuu ya utendaji ya chama cha PDP, mwezi Septemba walimtangaza Jonathan kugombea katika kinyang'anyiro hicho na kusema kuwa watamuunga mkono kama mgombea pekee.

Hata hivyo, Rais Jonathan ambaye alichukua madaraka mwaka 2010 baada ya kifo cha mtangulizi wake Umar Yar'Adua, amekuwa akikosolewa vikali na chama kikuu cha upinzani nchini Nigeria cha All Progressive Congress-APC.

Chama cha APC kimemkosoa kiongozi huyo wa Nigeria kutokana na kushindwa kudhibiti hali ya usalama pamoja kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram. Katika kipindi cha miaka mitano, nchi hiyo imewapoteza zaidi ya wananchi wake 10,000, huku baadhi ya miji ya kaskazini-mashariki ikidhibitiwa na waasi katika miezi ya hivi karibuni.

Viongozi wa chama cha APC, Muhammadu Buhari na Atiku Abubakar
Viongozi wa chama cha APC, Muhammadu Buhari na Atiku AbubakarPicha: Atiku Media Office

Jonathan atangaza nia wakati taifa halina usalama

Hatua ya Rais Jonathan kutangaza rasmi nia yake, imekosolewa vikali kutokana na shambulio lililofanyika jana Jumatatu katika shule moja na kuwaua kiasi wanafunzi 47. Mripuaji mmoja anayeshukiwa kuwa mfuasi wa Boko Haram, aliyejitoa muhanga, aliishambulia shule moja katika jimbo la Yobe, lililoko kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Kabla ya kuzungumza katika mkutano huo, Rais Jonathan alitangaza kuwepo ukimya kwa dakika moja ya kuwakumbuka wanafunzi waliouawa katika shambulio hilo. Amesema shambulio hilo limeitia doa nchi hiyo, lakini ana uhakika kwamba watashinda vita dhidi ya ugaidi.

Aidha, rais huyo anakosolewa kwa kushindwa kupambana na rushwa na utawala mbovu na uwajibikaji, hali ambayo wapinzani wake wanasema imekuwa mbaya zaidi tangu aliposhinda katika uchaguzi wa mwaka 2011.

Uchaguzi wa Nigeria, nchi yenye watu wengi barani Afrika na uchumi mkubwa na ambayo ni muuzaji wa juu wa mafuta tangu mwaka 2010, utafanyika Februari 14, mwakani, kumchagua rais mpya. Chama cha PDP kimekuwa madarakani tangu Nigeria iliporejea katika utawala wa kiraia mwaka 1999.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman