1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Karzai asema atampa ulinzi Mullah Omar

Kalyango Siraj17 Novemba 2008

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai yuko tayari kufanya mazungumzo ya amani na kiongozi wa kundi la Taliban Mullah Mohammed Omar.

https://p.dw.com/p/FwQf
Mullah Omar akionekana katika picha zilizochukuliwa wakati tofautiPicha: AP

Pia amesema kuwa ikiwa kiongozi huyo wa wapiganaji atakubali hilo, rais Karzai atamhakikishi ulinzi kwa ajili ya usalama wake.

Kauli ya rais Karzai ya kuzungumza na kiongozi wa wapiganaji wa Taliban ameitoa jana baada ya kukamilisha safari yake ya mbali iliompeleka Uingereza na Marekani.Ameongeza kuwa ikiwa atasikia kuwa kiongiozi huyo yuko tayari kwa majadiliano atampa ulinzi unaostahiki.'Nikipata ujumbe kutoka kwake kuwa yuko tayari kuja Afghanistan ama yuko tayari kufanya majadiliano ya amani kwa ajili ya watu wa Afghanistan,ili watoto wetu wasiendelee kuuliwa,basi mimi kama rais wa Afghanistan litafanya kila juhudi za kumlinda’,amesema Karzai.

Na leo jumatatu Wataliban wamesema kuwa wanatayarisha jibu la kauli ya rais Karzai.Katika kipindi kilichopita Wataliban wamekuwa hawataki kufanya mazungumzo yoyote ikiwa vikosi vya kigeni vikiwa baado katika ardhi ya Afghanistan.Rais Karzai akizungumza jana alisema sharti hilo halikubaliki.

Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid, akizungumza kwa simu na shirika la habari la Reuters akiwa mahali pasipojulikana, amekataa kutoa maoni kuhusu matamshi ya rais Karzai lakini akasema kuwa tamko lao litatolewa baadae jumatatu.

Hata hivyo tamko la rais Karzai kumuhusu Mullah Omar linakwenda kinyume na msimamo wa serikali ya Marekani ya sasa inayoongozwa na rais George W. Bush, ilioutoa mara ya mwisho mwezi Oktoba mwaka huu.Msimamo huo ni kuwa kiongozi wa Taliban asihusishwe katika juhudi zote za maridhiano.Lakini rais Karzai anaonekana anapinga wazo hilo.‚Nikisema kuwa nataka Mullah Omar apatiwe ulinzi,jamii ya kimataifa ina mawili ya kuchagua: aidha kuiniondoa madarakani ama kuniacha ikiwa hawakubaliani nalo.Mimi ni rais wa nchi hii.Kwa hivyo nikiamua kuwa hili lifanywe,jamii ya kimataifa ni lazima ikubaliane nami na ifanye hivyo.Ikiwa hawakubaliani nalo, basi wana njia nyingine yakutafakari’

Msimao huu wa kiongozi wa Afghanistan umekuja wakati ghasia nchini mwake zikiwa zimeongezeka katika kipindi cha miaka miwili iliopita na hivyo kuzusha hofu ya majaliwa ya serikali yake inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi pamoja na majaliwa ya taifa zima.

Wanajeshi wa kigeni takriban elf 70, ambao nusu yao ni kutoka Marekani, wanapambana dhidi ya wa Taliban ambao mashambulizi yao pamoja na mvuto vinasambaa katika maeneo ya kusini, mashariki na magharibi mwa nchi hiyo.

Rais mteule wa Marekani,Barack Obama nae pia ameonekana anapendelea mazungumzo na viongozi wa Kitaliban wenye msimamo wa kadri kuona kama mkakati wa Iraq unaweza ukafanya kazi hata nchini Afghanistan.Hatua ya kwanza ya mazungumzo ilifanyiwa majaribio mwezi Septemba wakati kundi la maafisa wanaopendelea serikali ya Afghanistan walipokutana nchini Saudia Arabia na maafisa wa zamani wa Taliban.

Lengo likiwa kutafuta njia za kukomesha mgogoro nchini mwao.Hata hivyo Taliban waliboronga mkutano huo kwa kurejelea kauli yao ya kuyataka majeshi ya kigeni kuondoka Afghanistan.