1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya Afrika ya Kati ataka vikosi zaidi

23 Januari 2014

Rais mpya wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza amesema idadi ya wanajeshi wa kimataifa waliopo nchini mwake haitoshi kurejesha utulivu katika mji mkuu, Bangui.

https://p.dw.com/p/1Avte
Rais mpya wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza anataka idadi ya wanajeshi wa kigeni iongezwe nchini mwake
Rais mpya wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza anataka idadi ya wanajeshi wa kigeni iongezwe nchini mwakePicha: Reuters

Rai ya rais Catherine Samba-Panza imetolewa katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Le Parisien la Ufaransa ambayo yamechapishwa katika toleo la leo Alhamisi. Katika mahojiano hayo Bi Samba-Panza amesifu mchango wa kijeshi wa Ufaransa ambayo ni mkoloni wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, na kuzitolea wito nchi nyingine za Ulaya kufuata mfano huo.

Catherine Samba Panza amesema kipaumbele chake mara tu atakapoanza kazi, ni kurejesha usalama nchini na kuweka mazingira ya kuwasaidia raia kurudi kazini.

Wakati huo huo mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na kuzuia mauaji ya halaiki, Adama Dieng amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuamuru hatua kubwa zaidi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kitisho cha mauaji ya halaiki

Akizungumza katika baraza hilo mjini New York jana, Dieng alisema nchi hiyo inakabiliwa na hatari kubwa ya ukiukaji wa haki za binadamu, na kutokea kwa mauaji ya halaiki.

Ghasia za kidini zinatishia kuitumbukiza Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mauaji ya halaiki
Ghasia za kidini zinatishia kuitumbukiza Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mauaji ya halaikiPicha: E.Feferberg/AFP/GettyImages

Adama Dieng alisisitiza juu ya umuhimu wa kutuma wanajeshi zaidi katika nchi hiyo haraka iwezekanavyo, kwani ni 4000 tu kati ya wanajeshi 6000 walioahidiwa kutoka nchi za kiafrika ambao wamekwishawasili.

Rais wa sasa wa Baraza la Usalama, mwanamfalme Zeid Ra'ad Zeid al-Hussein kutoka Jordan, amesema wanalaani uhalifu mpya unaofanyika kila siku katika Jamhuri ya Afrika ya kati, na kuahidi kuiunga mkono serikali mpya ya mpito. Hali kadhalika amesema baraza litaishughulikia haraka hali inayozidi kuwa mbaya nchini humo.

''Baraza litalifanyia kazi azimio linalohusu kuimarisha ofisi yetu kwa ajili ya amani na utengamano katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, mnamo siku chache zijazo.'' Alisema Zeid al-Hussein.

Damu yaendelea kumwagika

Mashahidi katika mji mkuu, Bangui, wamesema kuwa watu 10 waliuawa jana katika mapigano kati ya wanamgambo wa kikristo na waasi wa zamani wa Seleka ambao ni waislamu. Kwa mujibu wa mashahidi hao, ghasia zilianzia karibu na gereza na kambi ya jeshi ambayo inakaliwa na waasi wa Seleka mjini Bangui. Bi Samba-Panza anaishi umbali wa mita zisizozidi 100 kutoka mahali hapo.

Wanajeshi wa kigeni wakilinda usalama mjini Bangui
Wanajeshi wa kigeni wakilinda usalama mjini BanguiPicha: MIGUEL MEDINA/AFP/Getty Images

Samba-Panza anakabiliwa na kibarua kigumu katika kuyang'anya silaha makundi tofauti yanayohasimiana, na kuiunganisha tena jamii ya nchi yake. Kuchaguliwa kwake na bunge kulisifiwa ndani na nje ya nchi yake, lakini serikali yake italazimika kutegemea msaada kutoka nje kwa sababu hazina ya nchi kwa sasa ni tupu.

Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Bangui Dieudonne Nzapalainga na Imam Mkuu wa eneo hili, wamesema hivi karibuni kuwa maeneo makubwa ya nchi hiyo kwa sasa yako chini ya udhibiti wa wababe wa kivita.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE

Mhariri: Ssessanga Iddi