1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa FIFA kuchaguliwa Ijumaa

Admin.WagnerD22 Februari 2016

Kamati tendaji ya FIFA kukutana Jumatano kabla ya mkutano mkuu wa shirikisho hilo, kumchagua rais mpya wa FIFA.Timu mbili zinazoifuatilia Barcelona zateleza Uhispania ,wakati refa awa kivutio katika Bundesliga

https://p.dw.com/p/1HzzD
Schweiz FIFA Präsident Blatter tritt zurück
Picha: picture-alliance/dpa/E. Leanza

Kamati tendaji ya shirikisho la kandanda duniani FIFA inakutana siku ya Jumatano kabla ya mkutano mkuu , huku kukiwa na mabadiliko kadhaa pamoja na vikwazo tangu mkutano uliopita tarehe 29 Mei mwaka 2015.

Viongozi ambao hawatakuwapo katika mkutano huo ni pamoja na rais wa FIFA Sepp Blatter ambaye amepigwa marufuku na mkamu wa rais Michel Platini ambaye pia amefungiwa na Alfredo Hawit ambaye amepigwa marufuku na kwa sasa yuko korokoroni.

UEFA-Präsident Michel Platini
Rais wa UEFA Michel PlatiniPicha: picture-alliance/dpa/W. Bieri

Wajumbe wengine kutoka mkutano wa mwaka jana wameondolewa kwa sasa kupitia vyama vyao. Makamu wa rais mwandamizi Issa Hayatou anakuwa mwenyekiti akikaimu kiti cha rais.

Kamati tendaji kwa kawaida huwa ina wajumbe 25, pamoja na mjumbe mmoja wa ziada pamoja na katibu mkuu. Kutokuwapo kwa Blatter , Platini na Hawit kunapunguza idadi ya maafisa hadi 22 katika mkutano wa Jumatano. Blatter na Platini hawamo katika orodha ya FIFA ya kamati tendaji baada ya kupigwa marufuku na kamati ya maadili ya FIFA Desemba 21.

Shirikisho la soka la dunia FIFA litachagua rais mpya na kuimarisha mabadiliko makubwa katika mkutano wake mkuu siku ya Ijumaa ili kurejesha hali ya kuaminika tena. Mikutano mingine ni pamoja na ule wa shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA huku kukiwa na matumaini kwamba hakutakuwa na hatua nyingine za kukamatwa maafisa wa mashirika hayo kuhusiana na uchunguzi wa rushwa.

FIFA Jerome Champagne stellvertretende Generalsekretär
Jerome Champagne mgombea wa kiti cha urais FIFAPicha: Getty Images/AFP/J. Thys

Wakati huo huo uchunguzi wa Marekani umefichua rushwa iliyotapakaa katika soka hali iliyozidi kuchafua heba ya shirikisho linaloendesha mchezo huo duniani FIFA. Miongoni mwa wale waliokamatwa hadi sasa ni makamu wa rais 6 wa zamani wa FIFA. Maafisa nchini Uswisi pia wanaendelea na uchunguzi wao wakati shirikisho hilo la FIFA linachagua rais mpya.

Saxwale amkaribisha Infantino

Nae mgombea wa kiti cha urais wa FIFA Gianni Infantino amekubali mwaliko kutoka kwa mgombea mwenzake Tokyo Sexwale kutembelea nchini Afrika kusini na kufanya ziara katika kisiwa cha Robben, jela ya enzi za ubaguzi wa rangi nje kidogo ya mji wa Cape Town.

Infantino na Sexwale walitarajiwa kufanya ziara hiyo leo Jumatatu.

Timu ya kampeni ya Sexwale imesema mfanyabiashara huyo wa Afrika kusini amewaalika wagombea wote wanne lakini Sheikh Salman, mwanamfalme Ali na Jerome Champagne wamekataa mwaliko huo, kutokana na shughuli nyingi kabla ya uchaguzi wa hapo Ijumaa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu