1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Ufaransa Sarkozy aapishwa

Oummilkheir16 Mei 2007

Kizazi kipya chashika hatamu za uongozi nchini Ufaransa

https://p.dw.com/p/CB47
Rais mpya wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akimuaga mtangulizi wake Jacques Chirac
Rais mpya wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akimuaga mtangulizi wake Jacques ChiracPicha: AP

Rais mpya wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amekabidhiwa hatamu za uongozi hii leo na mtangulizi wake Jacques Chirac , akiugeuza ukurasa wa historia ya kisiasa ya nchi aliyoahidi kuifanyia mageuzi ya kina.

Sherehe za kukabidhiwa madaraka rais mpya wa Ufaransa Nicolas Sarkozy zimefanyika kama kawaida katika kasri la Elysée –kitovu cha madaraka nchini Ufaransa.

Nicolas Sarkozy,mwenye umri wa miaka 52 ,mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais May sita iliyopita dhidi ya mgombea wa chama cha kisoshialisti Ségolène Royal anashika hatamu za uongozi wa Ufaransa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo-akifungua enzi ya kizazi kipya madarakani.

Kama ilivyo desturi zulia jekundu limetandikwa katika uwanja wa heshima wa kuingia katika kasri la Elyseée ambapo rais anaemaliza mhula wake alimpokea na kumkaribisha ndani ya kasri hilo,Nicolas Sarkozy kwa mazungumzo yaliyodumu chini ya saa moja ambapo Nicolas Sarkozy alikabidhiwa ufunguo wa mtambo wa kinuklea wa Ufaransa na mtangulizi wake

Baadae wanasiasa wote hao wawili walirejea tena katika uwanja wa Elysée ambapo Jacques Chirac aliwaaga wafaransa na kulipa kisogo kasri la Elysée kama raia -mahala alikoishi kwa muda wa miaka 12.

Rais mpya wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameshaapishwa, sherehe zilizofuatiwa na kufyetuliwa mizinga 21- kwa mara ya 23 tangu mwaka 1848.

Kabla ya hapo rais mpya Nicolas Sarjkozy alisema:

„Hivi karibuni nitapitisha maamuzi muhimu kwa nchi yetu.Nitafanya hivyo kwa kuzingatia misingi ya mshikamano,haki na ujuzi.

Baada ya kuapishwa rais Sarkozy alisifu michango ya marais wote waliomtangulia,ikiwa ni pamoja na msoshialisti Francois Mitterand.Amesifu historia ya wafaransa na moyo wao wa mshikamano na udugu.

Rais mpya Nicolas Sarkozy anapanga kumteuwa Francois Fillon kua waziri mkuu mpya ,katika serikali itakayokua na mawaziri 15 tuu-nusu wakiwa wanawake.Ameshaahidi serikali hiyo mpya itawajumuisha wanasiasa wenye ujuzi bila ya kujali wanatokea chama gani.

Miongoni mwa wanaopigiwa upatu kuwa na nafasi nzuri ya kuchaguliwa ni msoshialisti Bernard Kouchner ,muasisi wa shirika la madaktari wasiojali mipaka.Duru za kuaminika zinasema huenda Bernard Kouchner akaukubali mwito huo licha ya lawama za chama chake cha kisoshialisti.

Wakati huo huo rais mpya wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anatazamiwa kuwasili Berlöin baadae hii leo kwa mazungumzo pamoja na kansela Angela Merkel wa Ujerumani.