1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Urusi ataendelea na siasa za kigeni

P.Martin2 Mei 2008

Juma lijalo,mwanasheria asie na uzeofu mkubwa katika sera za kigeni,atakuwa rais wa Urusi na atakuja kuiongoza nchi iliyo na silaha za nyuklia huku ikitegemewa na nchi za Magharibi kwa gesi na mafuta.

https://p.dw.com/p/Ds8n
Russian First Deputy Premier and presidential hopeful Dmitry Medvedev casts his ballot at a poling station in downtown Moscow Sunday, March 2, 2008. (AP Photo/Ivan Sekretarev )
Dmitry Medvedev atakaeapishwa rais mpya wa Urusi tarehe 7 Mei 2008.Picha: AP

Wanadiplomasia na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa kwa sehemu kubwa Dmitry Medvedev atakaeapishwa rais mpya wa Urusi tarehe 7 Mei, ataendelea na siasa za mtangulizi wake Vladimir Putin-siasa zilizowavutia wengi nchini Urusi na kuzishtusha nchi za Magharibi.Ingawa Medvedev alikuwa mshirika mkuu wa Putin tangu miaka mingi,si mengi yanayojulikana juu ya msimamo wake kuhusika na siasa za nje.Licha ya kuonekana kuwa msimamo wake unaelemea upande wa Magharibi,wachambuzi wanasema vitendo vyake ndio vitakavyokuja kudhihirisha ukweli.

Waziri Mkuu wa Luxembourg Jean-Claude Juncker aliekutana na Medvedev amesema,wakati wa mazungumzo yao ya faragha,kiongozi huyo alieleza mawazo yake kwa urefu.Juncker akaongezea kuwa Medvedev anataka kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wa Urusi na Ulaya.Hata hivyo,Juncker alie mmoja kati ya viongozi wachache wa kigeni kukutana na Medvedev tangu kiongozi huyo kuteuliwa rais wa Urusi,hatarajii kuona mabadiliko katika siasa za hivi sasa.Vladimir Putin akitazamiwa kuwa waziri mkuu,kuna wengi walio na shaka na kuuliza ikiwa Medvedev mwenye miaka 42 ataweza kujiimarisha au atakujamuigiza tu mkuu wake.

Miongoni mwa changamoto zinazomkabili Medvedev ni mradi uliopendekezwa na Marekani kuwa na mfumo wa ulinzi nchini Poland na Jamhuri ya Czeki kuzuia makombora,suala la upanuzi wa shirika la NATO,vishinikizo vya makundi yanayogombea kujitenga na Urusi,migogoro inayohusika na nishati na njia ya kuzuia mapambano ya wazi wazi pamoja na majirani kama Georgia - bila ya kuonekana kuwa dhaifu mbele ya umma ndani ya nchi.

Tangu mwaka 2000,Putin katika hotuba zake alikuwa akizishambulia nchi za Magharibi akitaka Moscow ipewe heshima.Ni dhahiri kuwa sera hizo zinapendwa na umma unaotaka kuhakikisha kuwa nchi hiyo haitopoteza usemi wake baada ya kusambaratika kwa iliyokuwa Soviet Union hapo mwaka 1991.

Kwa maoni ya Nikolai Zlobin wa Taasisi ya Usalama Duniani iliyo Washington,Marekani,Urusi itakuwa na mtazamo wa kirafiki kuhusu wawekezaji wa kigeni na majirani wake itakapokabiliwa na mporomoko wa uchumi wake na hadi hapo itakingwa na pato kubwa linalotokana na gesi na mafuta nchini humo.

Dmitry Medvedev amesema,ataizuru Kazakhstan iliyokuwa jamhuri ya Soviet Union ya zamani na baadae atakwenda China.Hizo zitakuwa ziara zake za kwanza baada ya kutawazwa rais wa Urusi Mei 7.