1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macri ahitimisha utawala uliogubikwa na migogoro

23 Novemba 2015

Rais mteule wa Argentina Mauricio Macris ameahidi kufufua uchumi wa taifa hilo ambao umekuwa ukiporomoka kwa kufanya mageuzi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kuboresha mfumo wa soko huru la biashara .

https://p.dw.com/p/1HAbI
Rais mteule wa Argentina Mauricio Macri
Rais mteule wa Argentina, Mauricio MacriPicha: picture-alliance/dpa/M: Di Maggio

Ushindi wa bwana Mauricio Macris umehitimisha utawala wa Rais Cristina Fernandez pamoja na marehemu mume wake katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliokuwa umegubikwa na migogoro.

Hata hivyo wakati Rais huyo mteule akiingia madarakani rasmi mnamo Dec. 10, mwaka huu ataanza majukumu yake huku akikabiliwa na changamoto ya mfumuko wa bei ya kwa kiwango cha asilimia 30 na matumizi makubwa ndani ya serikali huku pia akikosa idadi kubwa ya wabunge ya kumuwezesha kupitisha marekebisho atakayopendelea yafanyike.

" Macri ataanza majukumu yake katika mazingira magumu sana ya kisiasa, atakumbana na wakati mgumu katika kufanya maboresho katika nyanja za kiuchumi" anasema Daniel Kerner ambaye ni mshauri wa masuala ya kiuchumi.

Katika asilimia 98 ya kura zilizokwishahesabiwa tayari, katika uchaguzi huo uliofanyika siku ya jumapili, Macris alikuwa kashinda kwa asilimia 51.5 ukilinganisha na asilimia 48.5 ya mgombea wa chama tawala Daniel Scioli,ambaye tayari amekubali kushindwa katika uchaguzi huo.

Ushindi huu unakomesha kipindi cha hali mbaya ya kisiasa na kiuchumi nchini humo ikiwa ni pamoja na mahusiano hafifu yaliyokuwepo ya kidiplomasia miongoni mwa mataifa kadhaa ikiwemo Marekani.

"Leo ni siku ya kihistoria, na ni kipindi cha mabadiliko sasa" alisikika bwana Macri huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Wakati wa kipindi cha kampeni Bwana Macri aliahidi kuwa msikivu na mtendaji zaidi tofauti na ilivyokuwa wakati wa utawala wa Fernandez.

Aahidi kutolipiza kisasi

Akihutubia maelfu ya wafuasi wake siku ya jumapili, Bwana Macri alisema hatalipiza kisasi katika kipindi cha utawala wake bali atajikita katika mipango ya maendeleo ya taifa hilo.

" Najisikia mwenye furaha sana kwa sababu leo ndio tumehitimisha utawala wa kimafia" alisikika akisema Felisa Sanchez ambaye ni mfuasi wa Bwana Macri huku akipeperusha bendera ya taifa hilo.

Macri ambaye sasa ametimiza umri wa miaka 56 ameahidi pia kuvutia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya kodi zisizo za lazima katika maeneo kadhaa.

Hata hivyo anatarajiwa kupata upinzani mkubwa bungeni wakati atakapochukua hatua za maboresho hayo ya kiuchumi.

Rais huyo anatokea katika moja ya familia zenye utajiri mkubwa nchini humo na umaarufu wake aliupata zaidi kupitia katika masuala ya kandanda wakati alipokuwa Rais wa kilabu moja maarufu ya Boca Junior nchini humo.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/EAP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman