1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mteule wa Marekani Barack Obama achukua hatua za dharura za kiuchumi

Thelma Mwadzaya25 Novemba 2008

Rais mteule wa Marekani Barack Obama ameahidi kushirikiana na viongozi wa ulimwengu katika mapambano dhidi ya msukosuko wa fedha punde baada ya kuchagua kikosi chake cha maswala ya uchumi

https://p.dw.com/p/G1Ui
Rais Mteule wa Marekani Barack ObamaPicha: AP

Kundi hilo la wataalam linatarajiwa kuanza kazi ifikapo tarehe 20 mwezi Januari mwaka ujao.


Timothy Geithner aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha naye kiongozi wa Wizara hiyo wa zamani Larry Summers aliteuliwa kuwa mshauri wake mkuu wa maswala ya kiuchumi katika Ikulu ya Whitehouse. Kwa upande mwengine serikali ya Marekani iliipa Benki ya Citigroup inayokabiliwa na matatizo ya fedha msaada wa dola bilioni 20.Benki hiyo inazongwa na madeni japo ilishapata msaada wa dola bilioni 25 na ahadi za kusimamiwa deni lake la dola bilioni mia tatu na sita.


Mpango huo ulisababisha bei katika soko la hisa kuimarika nao wawekezaji wanaripotiwa kuipongeza hatua hiyo.


Wakati huohuo nchi ya Uingereza imetangaza mpango unaoazimia kuchagiza biashara vilevile kulisaidia taifa hilo kurejea katika hali ya kawaida huku uchumi ukitarajiwa kudorora ifikapo mwaka ujao.Mpango huo utagharimu paundi bilioni 20 za Uingereza.


Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha wa Uingereza Alistair Darling hatua zitakazochukuliwa zinajumuisha kufutilia mbali kodi za bidhaa na huduma pamoja na kuongeza kodi zinazolipwa na raia tajiri nchini humo ifikapo mwaka 2011.Bwana Darling kadhalika alipendekeza kuanzishwa kwa miradi mikubwa ya umma kama vile kuimarisha barabara kuu,ukarabati wa shule pamoja na nyumba. Miradi hiyo inatarajiwa kugharimu paundi bilioni 3.Alipendekeza pia kupunguzwa kwa kodi ya mauzo VAT ifikapo Disemba Mosi kutoka asilimia 17.5 hadi asilimia 15 kwa kipindi cha miezi 13.


Katika ripoti yake kabla ya kusoma bajeti Waziri huyo wa Fedha kwa upande mwingine alionya kuwa uchumi wa Uingereza utaathirika na hali hiyo haitobadilika hadi mwaka 2010.


Wawekezaji wanaripotiwa kupongeza hatua hiyo iliyosababisha bei ya hisa katika soko la Uingereza kuimarika.