1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mugabe na Tsvangirai kukutana wiki ijayo

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP15 Januari 2009

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai wiki ijayo atafanya mkutano na rais Robert Mugabe kujaribu kutatua mkwamo wa kisiasa uliko nchini humo.

https://p.dw.com/p/GZ6c
Morgan Tsvangirai,Kiongozi wa chama chama upinzani nchini Zimbabwe ,MDC (kushoto) na rais Robert Mugabe wa Zimbabwe(kulia).Picha: AP

Katika mkutano na waandishi wa habari nchini Afrika Kusini Tsvangirai amesema anamatumaini kuwa mkutano huo utazaa matunda, licha ya utawala wa rais Mugabe kuendelea kuwanyanyasa wapinzani na hata kukiuka makubaliano ya kugawana madaraka na upinzani.

Ombi hilo la kufanya mkutano kati yake na rais Mugabe halikufanya moja kwa moja bali kupitia rais wa Afrika Kusini Kgalema Motlanthe. Kwa mujibu wa msemaji wa rais Montlanthe,rais huyo alikubali kusaidia kufanikisha mkutano huo.Japokuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika mji mkuu wa Zimbabwe,Harare maelezo hayajatolewa kuhusu ni wapi mjini humo na wala utaandaliwa saa ngapi.

Tsvangirai anarejea nchini Zimbabwe siku ya jumamosi kwa matayarisho ya mkutano huo ambao swala kuu ni kujadili upya kutekelezwa kwa makubaliano ya kuundwa kwa serikali ya muungano.Makubaliano ya kugawana madaraka kati ya Tsvangirai na rais Mugabe mwezi september mwaka jana yamekwama huku wawili hao wakikosa kukubaliana kuhusu kugawana wizara muhimu.


Rais wa Afrika kusini Kaglema Motlanthe atakutana na viongozi hao wawili na kujaribu kuwapanisha.Tsvangirai pia amekuwa akimlaumu rais Mugabe kuhusu kuendelea kuzuiliwa na kuteswa kwa wafuasi wake.

Kiongozi huyo wa upinzani nchini Zimbabwe pia ameulaumu utawala wa Rais Mugabe kwa kusababisha mzozo wa kiutu,huku nusu ya idadi ya watu wakiwa hawana chakula na zaidi ya wazimbabwe 2,100 wakifariki kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Kipindupindu.

Serikali ya muungano kati ya rais Mugabe mwenye umri wa miaka 84 na Tvangirai ilibuniwa kufuatia utata uliozunguka uchaguzi mkuu wa mwaka jana nchini Zimbabwe.Mugabe alikuwa abakie rais huku Tsvangirai akichukua wadhifa uliobuniwa wa waziri mkuu.Makubaliano hayo pia yalitoa hakikisho kuwa vyama vya kisiasa vitaendesha shughuli zao bila kuingiliwa,swalaTsvangirai anasema limepuuzwa na serikali ya rais Mugabe.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya shirika la kimataifa la kutetea haki za kinadamu la Human Rights Watch wafuasi 32 wa upinzani na wanaharakati wa kisiasa wanazuiliwa nchini Zimbabwe kinyume cha sheria huku wengine 11 hawajulikani waliko.

Inadaiwa walitiwa mbaroni na polisi katika maeneo tofati tangu October mwaka jana na walianza kufikishwa mahakamani december 24 mwaka uliopita.Licha ya matatizo yanayoendelea kukumba Zimbabwe Afrika Kusini inaendelea kushikilia kuwa serikali ya kugawana madaraka na rais Mugabe ndio suluhu.

Miongoni mwa waliotiwa mbaroni ni maafisa wawili wakuu wa chama cha Movement for Democratic Chande -MDC wanaodaiwa kuwatisha polisi wanaochunguza mauji ya afisa mkuu wa jeshi la anga nchini Zimbabwe.Perrance Shiri aliuawa kwa kupigwa risasi december 10 mwaka jana,kutokana na kile maafisa wa serikali walisema ni mashambulizi dhidi ya utawala wa rais Mugabe.Shiri ni binamu ya rais Mugabe. .