1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mugabe wa Zimbabwe kugombea duru ya pili ya uchaguzi

5 Aprili 2008

Chama tawala cha ZANU-PF nchini Zimbabwe kimesema,Rais Robert Mugabe atagombea duru ya pili ya uchaguzi dhidi ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha MDC Morgan Tsvangirai.

https://p.dw.com/p/DcUP
Vtoile Silaigwana (C), deputy chief election officer of the Zimbabwe Electoral Commission (ZEC), reads the results of the House of Assembly election in Harare, capital of Zimbabwe, April 3, 2008. The ZEC announced the preliminary results of the House of Assembly election early on Thursday. The Zimbabwe African National Union-Patriotic Front (ZANU-PF) won fewer seats than the opposition Movement for Democratic Change (MDC) in the House of Assembly. Foto: Xinhua +++(c) dpa - Report+++
Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe ZEC ikitangaza matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa bunge ulioshindwa na chama kikuu cha upinzani cha MDCPicha: picture-alliance/ dpa

Tangazo hilo linadhihirisha kuwa chama tawala kinakiri hadharani kuwa Mugabe anaetawala tangu miaka 28 iliyopita hakufanikiwa kumshinda kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai wa chama cha MDC katika duru ya kwanza.Matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais uliofanywa tangu Jumamosi iliyopita yangali yakingojewa.

Kwa upande mwingine,mgogoro mpya umezuka kuhusu matokeo ya uchaguzi wa bunge ambao pia ulifanywa Jumamosi iliyopita.Ingawa chama cha MDC kilitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe kama mshindi wa uchaguzi wa bunge, chama cha Mugabe ZANU-PF kinapinga matokeo hayo.Chama cha Mugabe kinachotawala tangu miaka 28 iliyopita, kinataka kura zihesabiwe upya katika wilaya 16.

Wakati huo huo chama cha MDC kimedai kuwa Morgan Tsvangirai amemshinda Mugabe katika uchaguzi wa rais.Hii leo mawakili wa MDC wanakwenda mahakamani mjini Harare kwa azma ya kuwahimiza maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanywa tangu juma moja lililopita.

Zimbabwe ambayo hapo zamani ilikuwa ikiyalisha mataifa mengine barani Afrika,leo hii inaagizia chakula kutoka nje na hutegemea msaada kuwalisha wananchi wake.Uchumi wa nchi hiyo umeporomoka vibaya mno.Wazimbabwe wanapambana na ughali wa maisha uliopindukia asilimia 100,000 na idadi ya watu wasio na ajira ni zaidi ya asilimia 80.