1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Musharraf aambiwa aondoke madarakani

20 Februari 2008

Chama cha PPP cha waziri mkuu wa zamani wa Pakistan alieuawa, Benazir Bhutto,kinajaribu kuunda serikali ya mseto itakayoweza kumuondosha madarakani Rais Pervez Musharraf.

https://p.dw.com/p/DAcs

Lakini Rais Musharraf hii leo alipinga kabisa mito ya kumtaka angatuke madarakani na badala yake alitoa mwito wa kuunda serikali ya mseto yenye utulivu.Hayo ni matamshi rasmi ya mwanzo kutolewa na Musharraf tangu washirika wake kushindwa vibaya katika uchaguzi mkuu uliofanywa siku ya Jumatatu nchini Pakistan.Sasa wadhifa wake wa urais upo hatarini.Kwani mjane wa Benazir Bhutto,Asif Ali Zardari wa chama cha PPP na waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif aliepinduliwa na Musharraf katika mwaka 1999 wamesema,wao wanataka kuunda serikali pamoja na vyama vingine vya upinzani.Nawaz Sharif amemuhimiza Musharraf ajiuzulu.Na Zardari alieshika uongozi wa chama cha PPP baada ya kuuawa kwa Benazir Bhutto mwishoni mwa mwezi wa Desemba amesema,hatofanya kazi na ye yote aliehusika na chama kilichomuunga mkono Musharraf katika serikali iliyopita.Vile vile chama cha PPP kilikumbusha matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Musharraf kuwa atajiuzulu iwapo vyama vinavyomuunga mkono,vitashindwa uchaguzi.Licha ya kushinikizwa,Musharraf amesema yeye hana mipango yo yote ya kujiuzulu.

Wakati huo huo,Rais George W.Bush wa Marekani amesifu uchaguzi wa Pakistan kama ni ushindi muhimu kwa demokrasia na amesema ni matumaini yake kuwa serikali mpya itakuwa rafiki wa Marekani.Itakumbukwa kuwa Musharraf ni mshirika mkuu wa Kiislamu wa Marekani katika vita dhidi ya mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.

Hata hivyo uchunguzi wa maoni uliofanywa nchini Pakistan kabla ya uchaguzi wa Jumatatu,umeonyesha kuwa hadi asilimia 75 ya wananchi waliohojiwa wamesema,wakati umewadia kwa Musharraf kuondoka madarakani.Kimsingi, vyama vinavyompinga Musharraf vikipata uwingi wa theluthi mbili bungeni basi vitaweza kufungua mashtaka dhidi ya Rais Musharraf.

Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, Musharraf huenda akatumia uhasama uliokuwepo hapo zamani kati ya chama cha Bhutto na Nawaz Sharif na hivyo akajaribu kuvitenganisha vyama hivyo viwili vinavyotazamia kuunda serikali ya mseto.