1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Musharraf ashinikizwa kurejesha demokrasia

7 Novemba 2007

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan,Benazir Bhutto amewasili Islamabad kujadiliana na viongozi wa upinzani,lakini amefutilia mbali kukutana na Rais Jemadari Pervez Musharraf.

https://p.dw.com/p/C77B

Bhutto ameungana na Jaji Mkuu alieachishwa kazi,Iftikhar Chaudhry kutoa mwito kwa umma kufanya maandamano bila ya kujali polisi,mpaka amri ya hali ya hatari itakapoondoshwa.Alipowasili Islamabad Bhutto alisema:

„Musharraf anapaswa kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa taifa na chama changu kuwa atajiuzulu kama mkuu wa majeshi.Pia kuna masuala mengine kama kuacha kuvikaba vyombo vya habari,kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa na kuheshimu utawala wa kisheria.Naishukuru jumuiya ya kimataifa kwa kuunga mkono demokrasia.Hata hivyo,shinikizo, ndani ya nchi na duniani,ziendelee mpaka hali ya utulivu itakapopatikana nchini Pakistan.“

Duru za upinzani zinasema,hadi wanasheria 3,500 waliyoongoza maandamano nchini Pakistan wametiwa mbaroni.Viongozi wa Ulaya wamelaani ukandamizaji huo na wametoa mwito kwa Rais Musharraf kuondosha amri ya hali ya hatari na kuacha madaraka yake kama mkuu wa majeshi.Marekani nayo imesema,hatua ya Musharraf kutangaza hali ya hatari ni kosa.