1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Nicolas Sarkozy aanza ziara nchini Urusi

9 Oktoba 2007

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa leo anaelekea nchini Urusi ambako anatarajiwa kupalilia uhusiano mpya wa kirafiki baina ya Ufaransa na Urusi nchi ambayo tayari ameishutumu kwa uvunjaji wa haki za binadamu pamoja na kuvuruga maswala ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/C7iL
Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa
Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: AP

Katika ziara yake hiyo rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anatarajiwa kukutana na rais Vladimir Puttin wa Urusi katika mkutano ambao unadhaniwa utagubikwa na mioto.

Kwani tangu alipochaguliwa mwezi Mei rais Sarkozy amekuwa anaishutumu Urusi kuhusu maswala ya haki za binadamu na pia jinsi Urusi inavyotumia utajiri wake wa mafuta kuwaonea majirani zake wa barani Ulaya huku ikitafuta kurejesha uhusiano mzuri na Marekani.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy alipokuwa ziarani mjini Sofia huko nchini Bulgaria wiki iliyopita aliishutumu Urusi kwa kuongeza matatizo duniani na akaikumbusha kwamba mataifa makubwa sio kuwa na haki tu bali yanahitaji pia kubeba majukumu.

Licha ya shutuma zote hizo viongozi hao wa Urusi na Ufaransa ambao kwa mara ya kwanza walikutana katika mkutano wa nchi nane tajiri kiviwanda wa G8 uliofanyika mjini Heiligendam hapa nchini Ujerumani mwezi Juni hawajakiri kwamba kuna mvutano wa kidiploamsia kati yao.

Wadadisi wanasema hali ya kupimana nguvu huenda ikajitokeza pale viongozi hao watakapo kutana katika dhifa ya chakula cha jioni mjini Moscow.

Swala kubwa ambalo linatabiriwa kujitokeza ni kuhusu uhuru wa jimbo wa Kosovo ambao unaungwa mkono na Ufaransa lakini unapingwa vikali na Urusi.

Iran pia ni swala jingine ambalo Ufaransa na Urusi hazikubaliani katika misimamo yao hasa pale Urusi inapokataa kuunga miito ya Marekani na Ulaya ya kutaka Iran iwekewe vikwazo vipya kwa ajili ya kuishinikiza iache mpango wake wa nyuklia.

Kwa upande wake Moscow imesema kwamba ziara hii ya kiongozi wa Ufaransa inatarajiwa kuuweka wazi msimamo wa nchi hiyo kuhusu maswala kadhaa ya kimataifa ikizingatiwa kauli zisizo lingana zinazotolewa na viongozi wa Ufaransa mara kwa mara.

Ziara ya rais wa Ufaransa nchini Urusi inakwenda sambamba na kutimia mwaka mmoja tangu mwandishi wa habari Anna Politikovskaya alipouwawa.

Mwanahabari huyo alikuwa mkosoaji mkubwa dhidi ya utawala wa Kremlin na hasa alipenda kuchapisha maovu yaliyotokea katika jimbo la Chechnya.

Rais Nicolas Sarkozy mara kwa mara amelaumu kampeni za jeshi la Urusi katika jimbo hilo.

Kwa upande wa kibishara Urusi na Ufaransa zinatarajiwa kuimarisha uhusino wao ilivyo kwamba makampuni makubwa ya mafuta ya nchi hizoTotal ya Ufaransa na Gazprom ya Urusi yanapanga kushirikiana katika biashara ya gesi na wakati huo huo shirika la ndege la Aeroflot la Urusi linapanga kununua ndege 22 kutoka kwenye kampuni ya Airbus.

Mipango mipya ya biashara itakayo jadiliwa na viongozi hao ni pamoja na uwezekano wa kushirikiana kwa kampuni kubwa za kutengeneza ndege, EADS ya Ulaya na UAC ya Urusi.