1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ziarani Afrika kusini

Hamidou, Oumilkher28 Februari 2008

Sarkozy anasema mikataba yote ya kijeshi pamoja na Afrika itadurusiwa.

https://p.dw.com/p/DFIK
Rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: AP


Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amewasili Afrika kusini hii leo kwa ziara rasmi ya siku mbili.Mara tuu baada ya kuwasili kiongozi huyo wa Ufaransa alikutana na mwenyeji wake, rais Thabo Mbeki na kuzungumzia zaidi

 mzozo wa nishati wa dola hilo kuu la kiuchumi barani Afrika.



Mwishoni mwa mazungumzo yao viongozi hao wawili walizungumza na  waandishi kabla ya kuhutubia kwa pamoja bunge la nchi hiyo.


Katika mkutano huo pamoja na waandishi habari rais Nicolas Sarkozy amesema ataliarifu bunge la Afrika kusini azma ya nchi yake ya kudurusu mikataba yote ya kijeshi iliyofikiwa kati ya nchi za kiafrika na Ufaransa.


Ameahidi pia mikataba yote mipya itafafanuliwa na kuachwa wazi". Rais huyo wa Ufaransa ameongeza kusema tunanukuu:"viongozi wote wa Afrika wamearifiwa juu ya azma hiyo."Mwisho wa kumnukuu.


Rais Thabo Mbeki amefurahishwa na tangazo hilo na kusema tunanukuu:"Ni sehemu ya utaratibu wa kuitakasa Afrika na mabaki ya ukoloni."Mwisho wa kumnukuu.


Rais Nicolas Sarkozy amefuatana na ujumbe mkubwa wa viongozi wa makampuni muhimu ya Ufaransa ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wa kampuni kubwa kabisa la nishati ya kinuklea AREVA bibi Anne Lauvergeon na mwenzake wa kampuni la umeme EDF,Pierre Gadonneix.Makampuni hayo ya Ufaransa yametoa ombi la kujenga mitambo miwili ya nishati ya kinuklea nchini Afrika kusini.


Katika mahojiano yaliyochapishwa na gazeti la Star la Afrika kusini hii leo,rais Sarkozy ameitaja sekta ya nishati kua ni miongoni mwa mhimili madhubuti wa uhusiano wa pande mbili.


Rais Thabo Mbeki na mgeni wake wa Ufaransa wanatazamiwa kutia saini makubaliano kadhaa kuhusu nishati,sayansi na teknolojia pamoja pia na ushirikiano katika sekta ya utalii,na usalama katika shughuli za usafiri-kwa kuzingatia  michuano ya fainali za kombe la dunia la kabumbu mwaka 2010 nchini Afrika kusini.


Rais Thabo Mbeki na kiongozi mwenzake wa Ufaransa Nicolas Sarkozy wanatazamiwa pia kuzungumzia mageuzi katika Umoja wa  mataifa na taasisi za fedha za kimataifa za Bretton Woods.


 Ufaransa ni mshirika wa nane wa kiuchumi kwa Afrika kusini na mteja mmoja wapo muhimu pia.Biashara ya pande mbili imefikia yuro bilioni mbili nukta mbili mwaka jana.


Nicolas Sarkozy anaefuatana na mkewe mpya,Carla Bruni amepangiwa pia kuzungumza na mwenyekiti wa chama cha Afrika National Congress Jacob Nzuma.


Baada ya kuhudhuria kongamano la kiuchumi la nchi hizi mbili kesho mjini Cape Town,rais Sarkozy na mkewe wanatazamiwa kwenda Johannesburg kwa ziara ya kibinafsi ambako watakutana na rais mstaafu wa Afrika kusini Nelson Mandela.


Hii ni ziara ya kwanza ya rais Nicolas Sarkozy katika nchi ya kiafrika inayozungumza kiengereza tangu alipokabidhiwa madaraka mwezi June mwaka jana.




►◄