1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama ataka "kusikiliza"Mashariki ya Kati

20 Machi 2013

Rais Barack Obama wa Marekani atawasili hivi punde Tel-Aviv -ziara yake ya kwanza nchini Israel itakayomfikisha pia katika ukingo wa magharibi na Jordan.

https://p.dw.com/p/180bx
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: Reuters

Rais Barack Obama anawasili Israel hii leo bila ya mpango wowote mpya wa amani.Amedhamiria kuanzisha msingi wa aina mpya katika uhusiano wake pamoja na waisrael na wapalestina.

Rais Barack Obama anaefuatana na waziri wake mpya wa mambo ya nchi za nje John Kerry atakutana sio tu na waziri mkuu Benjamin Netanyahu bali pia na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palestina Mahmud Abbas.

Amepangiwa pia kuwahutubia moja kwa moja waisrael katika hotuba atakayoitoa mbele ya wanafunzi.Anatarajiwa pia kuitembelea Jordan.

Duru za kuaminika zinasema rais Obama atarajibu kuwatanabahisha waisrael na wapalastina warejee tena katika meza ya mazungumzo ya amani.Atajaribu pia kumtuliza Benjamin Netanyahu aliyepania kuizuwia Iran isimiliki bomu la kinuklea.Suala la vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Irak nalo pia litajadiliwa.

Hakuna lakini anaetegemea mepya katika ziara hii ya siku tatu inayopewa sifa ya" ziara ya aina yake."

Bendera za Marekani na zile za Isreal zimetundukiwa majiani mjini Jerusalem pamoja na biramu zinazosifu uhusiano "usiotetereka" kati ya nchi hizo mbili.

Mara tu baada ya kuwasili rais Barack Obama amepangiwa kuukagua mtambo wa kinga dhidi ya makombora Iron Dome unaoagharimiwa na Marekani.Mtambo huo umelenghwa kuwakinga waisarael na hujuma za makombora yanayofyetuliwa kutoka Gaza.

Viongozi watakiwa wawe na subira

Jerusalem's Erwartungen an Barack Obama
Wakaazi wa Jerusalem waelezea matumaini yao kuhusu utaratibu wa amani ya mashariki ya katiPicha: DW/D. Cheslow

Baadae hii leo rais Obama na waziri wake wa mambo ya nchi za nje John Kerry watazungumza kwa muda mrefu na waziri mkuu Benjamin Netanyahu.Duru zinasema viongozi hao watajaribu kuepukana na mivutano iliyoshuhudiwa wakati wa mikutano yao ya miaka iliyopita.

Iran pia ni miongoni mwa mada mazungumzoni.Marekani na Israel zinakubaliana Iran haistahiki kumiliki bomu la kinuklea,lakini washirika hao wawili wanatofautiana juu ya hatua zinazobidi kuchukuliwa.Inasemekana rais Obama atawasihi waisrael wawe na subira.Washington inahofia hujuma za kijeshi za Israel zinaweza kuitumbukiza Marekani katika vita vyengine vya Mashariki ya kati.

Barack Obama aliyesema anakuja Mashariki ya kati" ili kusikiliza",amepangiwa kwenda kesho kwa mazungumzo pamoja na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palestina Mahmoud Abbas.

Jana machafuko yaliripuka katika mji huo kati ya plisi na waandamanaji wanaopinga ziara hiyo ya rais Obama .

Mandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman