1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lengo ni kuwakabili taliban na kuwalinda raia.

Abdu Said Mtullya2 Desemba 2009

Marekani itapeleka wanajeshi zaidi nchini Afghanistan lakini inakusudia kuondoka mnamo mwaka 2011.

https://p.dw.com/p/KnMI
Rais Barack Obama ametangaza hatua ya kupeleka majeshi zaidi nchini Afghanistan.Picha: AP

NEW YORK:

Rais Barack Obama ametangaza kwamba Marekani inapeleka askari 30,000 zaidi nchini Afghanistan kwa lengo la kuimarisha mapambano dhidi ya wapinzani wa kitaliban ambao amesema wameimarika.

Akihutubia kwenye chuo cha mafunzo ya maafisa wa kijeshi cha West Point, rais Obama alisema kuwa hatua aliyoamua kuchukua pia itasaidia kuleta mazingira yatakayowezesha kulihamishia jukumu la ulinzi katika mikono ya serikali ya Afghanistan.

Obama amesema lengo la kuongeza wanajeshi ni kupambana na alkaida,kuwalinda wananchi pamoja na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wazalendo wa Afghanistan.

Rais Obama ameeleza kwamba Marekani inapeleka majeshi zaidi nchini Afghanistan ili kuionyesha dunia kwamba lengo lake ni halali na kwamba dhamira ya nchi hiyo haitatetereka.

Hatahivyo Marekani itaanza kuondoka Afghanistan mwezi julai mwaka 2011 kabla ya kumalizika kwa muhula wa rais Obama.