1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama awasili Saudi Arabia.

Sekione Kitojo3 Juni 2009

Rais Barack Hussein Obama amekutana na mfalme Abdullah wa Saudi Arabia leo baada ya kuwasili nchini humo kuanza ziara yake ya mataifa ya mashariki.

https://p.dw.com/p/I2yb
Rais Barack Obama anashikana mkono na mfalme wa Saudi Arabia baada ya kupokea zawadi kutoka kwa mfalme Abdullah mwanzoni mwa ziara yake ya mashariki ya kati.Picha: AP

Rais Barack Obama amekutana hii leo na mfalme wa Saudi Arabia , mfalme Abdullah mjini Riadh kabla ya hapo kesho kutoa hotuba yake muhimu ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa mjini Cairo, ambayo kiongozi huyo wa Marekani ana matumaini kuwa itakarabati hadhi ya Marekani iliyoharibika katika ulimwengu wa mataifa ya Kiislamu.

Baada ya kulakiwa katika uwanja wa ndege wa Riadh, Obama alisafiri hadi katika shamba la mfalme Abdullah ambako viongozi hao wawili walifanya mazungumzo yaliyotarajiwa kuangalia suala la mzozo kati ya Waarabu na Israel, pamoja na mazungumzo ya awali na Iran pamoja na suala la mafuta.

Muda mfupi baada ya Obama kuwasili , televisheni ya Al Jazeera ilirusha hewani maelezo ya kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda Osama bin Laden ambamo alisema rais huyo wa Marekani anapanda mbegu kwa ajili ya kulipiza kisasi pamoja na chuki , kuelekea Marekani katika ulimwengu wa mataifa ya Kiislamu.

Bin Laden amesema Obama anaendeleza hatua za mtangulizi wake George W. Bush na kuwaambia Wamarekani kujiweka tayari kwa matokeo ya siasa za ikulu ya Marekani.

Obama ambaye baba yake alikuwa Muislamu na ambaye aliishi nchini Indonesia akiwa kijana mdogo, anamatumaini ya kuitengeneza hadhi ya Marekani ambayo ilichafuliwa na vita vilivyoanzishwa na rais Bush nchini Iraq na Afghanistan pamoja na jinsi Marekani ilivyokuwa ikiwashughulikia mateka wao wa vita hivyo.

Rais Obama anatarajiwa kulala hadi kesho nchini Saudi Arabia kabla ya kwenda mjini Cairo kwa ajili ya hotuba yake muhimu kuelekea ulimwengu wa Kiislamu, ambapo atatimiza ahadi yake wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana kuwa atahutubia kutoka katika mji mkuu wa nchi ya Kiislamu mapema katika utawala wake.

Mwanadiplomasia mmoja wa Iran amesema kuwa Misr mwenyeji wa rais Obama imemwalika mwanadiplomasia wa ngazi ya juu kutoka Iran kuhudhuria hotuba hiyo.

Kuijumisha Iran katika waalikwa katika hotuba ya rais Obama ni muhimu kwa kuwa Iran na Marekani hazina uhusiano wa kibalozi, na maafisa kutoka nchi hizo mbili kwa kawaida hujiepusha kukutana.

Lakini mashambulio mara mbili kutoka kwa al-Qaeda dhidi ya Obama yanaoyesha kuwa kundi hilo lina wasi wasi mkubwa kuhusiana na uwezo na mbinu za ushawishi za rais wa Marekani Barack Obama.

Kiongozi wa al-Qaeda amemshambulia rais Obama leo Jumatano katika matamshi yake mapya kabisa, lakini jana kiongozi namba mbili Ayman al-Zawahiri alitoa matamshi pia ya kumshambulia rais Obama. Mtazamo wa rais Obama ni kuunganisha pande hizi mbili ambazo haziaminiani.

Zawahiri anahaki ya kuwa na wasi wasi, amesema Edwin Bakker, mtafiti mwandamizi katika taasisi ya Clingendael mjini The Hague nchini Uholanzi. Kundi la al-Qaeda linaishi kutokana na kuwapo chuki dhidi ya Marekani na vita dhidi ya ugaidi. Hivi sasa rais Bush ameondoka na nafasi yake imechukuliwa na mtu ambaye jina lake la kati ni Hussein, na wanahofia kuwa hotuba yake inaweza kuwa na athari nzuri.

►◄



Mwandishi : Sekione Kitojo/RTRE

Mhariri Mohammed Abdul Rahman