1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama awasili Tokyo

Kabogo Grace Patricia13 Novemba 2009

Akiwa huko atakutana na Waziri Mkuu wa Japan, Yukio Hatoyama.

https://p.dw.com/p/KVwg
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani leo amewasili mjini Tokyo, Japan ikiwa ni ziara yake ya kwanza barani Asia tangu alipoingia madarakani, ambapo baadaye leo atakutana na Waziri Mkuu wa Japan, Yukio Hatoyama.

Ndege ya rais Air Force One, ilitua katika uwanja wa ndege wa Tokyo kabla Rais Obama hajakutana na Hatoyama ambaye ameahidi kuilekeza nchi yake katika njia iliyo huru na kuzusha wasi wasi na ushirikiano wa karibu nusu karne.

Rais Obama ambaye yuko katika ziara hiyo bila mkewe, Michelle Obama, alilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Japan, Katsuya Okada na Balozi wa Marekani nchini Japan, John Roos. Akizungumzia ziara yake hiyo Rais Obama alisema:

''Kumbukumbu za Hiroshima na Nagasaki bado zinaendelea kuwepo katika mawazo ya walimwengu na nitapata heshima ya kutembelea maeneo ya miji hiyo katika ziara yangu hii nikiwa rais.''

Yatakayozungumzwa

Nchini Japan ambako serikali mpya iliingia madarakani miezi miwili iliyopita, Rais Obama na Hatoyama watazungumzia masuala kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, vita vya Afghanistan na dunia isiyo na silaha za nyuklia, ikiwemo vitisho vinavyowekwa na Korea Kaskazini, ambayo siku za nyuma ilifanya majaribio ya makombora katika visiwa vya Japan.

Msemaji wa ngazi ya juu wa Serikali ya Japan, Hirofumi Hirano, amesema viongozi hao wawili watazungumzia pia zaidi juu ya kuimarisha uhusiano baina ya Hatoyama na Obama na nchi zote mbili kwa ujumla. Awali Hatoyama alisema huenda akafutilia mbali mpango usioungwa mkono wa kujenga ngome mpya ya jeshi la Marekani katika kisiwa cha kusini cha Okinawa na kwamba ataachana na kupeleka kikosi cha jeshi la wanamaji ambacho tangu mwaka 2001 kimekuwa kikiunga mkono kampeni za Marekani nchini Afghanistan. Akisisitizia juu ya misaada ya kibinaadamu, serikali ya Hatoyama wiki hii iliahidi kutoa dola bilioni tano kwa ajili ya kusaidia kudhibiti vita nchini Afghanistan ambayo ni changamoto kubwa ya Rais Obama katika sera zake za kigeni.

Nchi nyingine atakazozitembelea

Katika ziara yake hiyo barani Asia itakayozihusisha nchi nne, Rais Obama kwa mara ya kwanza atakutana na viongozi wengi wa eneo hilo katika mkutano wa wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Nchi za Asia na Pasific-APEC, unaofanyika Singapore. Rais Obama pia atakuwa ni rais wa kwanza wa Marekani kukutana pamoja na viongozi 10 wa APEC, ikiwemo nchi ya Myanmar ambayo ni adui wa Marekani.

Baada ya hapo Rais Obama ataelekea China ambapo akiwa huko atazungumzia masuala mbalimbali yanayoihusu dunia nzima, biashara na tofauti za sarafu. Aidha, akiwa nchini China Rais Obama atakutana na kaka yake Mark Ndesandjo na mkewe ambaye ni raia wa China. Rais Obama kisha ataelekea Korea Kusini, ambako katika mahojiano yake na shirika la habari la nchi hiyo, Rais Obama amesema Korea Kaskazini ni tishio, lakini akaongeza nchi hiyo ina nafasi na kuimarisha sura yake katika jumuiya ya kimataifa endapo itaachana na mpango wake wa nyuklia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri: M.Abdul-Rahman