1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama leo anakutana na Dalai Lama.Nini kitatokea baada ya mkutano huo?

Abdu Said Mtullya18 Februari 2010

Jee uhusiano wa Marekani na China utakuaje baada ya rais Obama kukutana na Dalai Lama ?

https://p.dw.com/p/M4Vb
Kiongozi wa kidini anaepigania haki za jimbo la Tibet, Dalai Lama.Picha: DW

Kiongozi wa kidini anaepigania haki za jimbo la Tibet, Dalai Lama, leo anakutana na rais Barack Obama katika Ikulu ya Marekani kama ilivyopangwa, licha ya upinzani mkali wa China.Jee uhusiano wa Marekani na China utakuaje baada ya mkutano huo ?

Mwandishi wetu Christina Bergmann anasema katika makala ifuatayo kwamba hapatatokea mawimbi ya kuzamisha meli. Safari hii Marekani haitageuka nyuma!Licha ya malalamiko ya China, rais Obama leo atakutana na kiongozi wa kidini anaepigania haki za watu wa jimbo la Tibet, Dalai Lama. Obama,

Msemaji wa Ikulu ya Marekani ameeleza, kuwa rais Obama anasubiri kwa hamu kubwa kukutana na Dalai Lama.Hapo awali, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China aliitaka Marekani ibatilishe ziara ya kiongozi huyo wa kidini.

Katika mwaka wake wa kwanza madarakani, rais Obama alitaka kufanya kila kitu tofauti na marais waliotangulia ambao katika kampeni za uchaguzi waliazimia kuonyesha msimamo mkali dhidi ya China.Lakini kutokana na mazingira yaliyofuatia uchaguzi wake, rais Obama alijikuta analazimika kufanya mazungumzo na China.

Mgogoro mkubwa wa fedha ulioikumba dunia uliwaleta pamoja kwenye mkutano, viongozi wa Marekani na China. Pia yafaa kutilia maanani kwamba China inamiliki dhamana za serikali ya Marekani, thamani ya dola bilioni 900.Kwa usemi mwingine, China ni mkopeshaji mmojawapo mkuu wa Marekani.

Ziara ya kwanza nje ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani,Hillary Clinton, ilikuwa nchini China. Katika ziara hiyo, bibi Clinton hakulipa kipaumbele suala la haki za binadamu ili kuweza kuyazingatia masuala mengine muhimu zaidi. Ni wazi kwamba alilaumiwa sana nchini Marekani.Rais Obama pia alilaumiwa kwa kukataa kukutana na Dalai Lama mwaka jana. Na hata alipofanya ziara ya China, Obama aliipanga ziara hiyo kwa kuwafiki kabisa na matakwa ya China.

Kwenye mkutano na wanafunzi waliochaguliwa mahsusi kukutana naye, Obama alisisitiza ushirikiano na China katika juhudi za kuyatatua masuala ya kiuchumi,hali ya hewa na upunguzaji wa silaha za nyuklia.

Lakini ukurasa mwingine wa uhusiano umefunguka kati ya Marekani na China.Katika ziara yake nchini Ufaransa,waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton,alisema China lazima ijiunge na msimamo wa nchi zinazotaka vikwazo madhubuti viwekwe dhidi ya Iran, la sivyo China itajitengakidiplomasia na itapunjika kiuchumi.

Hatua nyingine ya mkwaruzano katika uhusiano wa China na Marekani ni uamuzi wa utawala wa Obama wa kuiuzia silaha Taiwan thamani ya dola bilioni 6.4 .

Na leo rais Obama anakutana na Dalai Lama.Maana yake nini?Mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa China na Marekani, Hachigan Gian, ameeleza kuwa matukio hayo yalitazamiwa.Amesema katika uhusiano wa nchi hizo panatokea mivutano ya mara kwa mara, lakini haitakuwa sawa kupiga chuku. Amesema hapatatokea mawimbi ya kuizamisha meli.

Mwandishi/Bergmann Christina/ZA/AFPE/

Imetafsiriwa na Mtullya Abdu/

Mhariri: Miraji Othman