1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama ziarani Mexico

Halima Nyanza/(Reuters) 16 Aprili 2009

Rais Barack Obama leo anaanza ziara nchini Mexico, ziara ambayo imeelezwa kuonesha mshikamano na jirani zake pamoja na kuthibitisha kuwa Marekani iko makini katika kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya na silaha.

https://p.dw.com/p/HYVL
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AP

Akiwa nchini Mexico leo Rais Barack Obama atasisitizia ushirikiano wa mipaka kati ya nchi hizo mbili na kulenga pia suala la nishati isiyoharibu mazingira.

Lakini hata hivyo, mazungumzo kuhusiana na mzozo wa Kiuchumi na Biashara ya dawa za kuleva, yameelezwa kuwa ndio yatakayotawala, hususan ikizingatiwa kuwa, asilimia 80 ya bidhaa ambazo Mexico inasafirisha nje imekuwa ikizipeleka kwa jirani zake Marekani na Canada.


Rais Rais wa Marekani atafanya ziara nchini Mexico kwa mazungumzo na mwenyeji wake Rais Felipe Calderon, akiwa njiani kuelekea Trinidad na Tobago kushiriki katika mkutano wa tano wa America utakaofanyika Ijumaa.


Utawala wa Rais Barack Obama umekuwa ukidhibiti sana mpaka katika ya Marekani na Mexico ili kuzuia biashara ya magendo ya silaha na unatarajia kutuma helikopta kwa ajili ya kumsaidia Rais wa nchi hiyo kupambana na makundi yenye silaha yanayojishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya, ambayo katika kipindi cha mwaka uliopita, magenge hayo yaliua maelfu ya watu.

Takriban watu elfu 6 300 waliuawa mwaka uliopita nchini humo na kwamba ghasia hizo zimeanza kuenea pia nchini Marekani.


Rais Obama, kutoka katika chama cha Democrat, anamatumaini ya kuimarisha uhusiano na Mexico pamoja na nchi nyingine za Latin America wakati wa ziara yake hiyo baada ya kupungua kwa uhusiano, ambapo wasaidizi wake wanamtupia lawama Rais aliyemaliza muda wake Mrepablican George W Bush.


Wakizungumzia ziara hiyo ya Rais Obama nchini Mexico, maafisa wa Ikulu ya Marekani walisema ziara hiyo ni ishara ya kumuunga mkono Rais Felipe Calderon na juhudi zake hizo za kukabiliana na makundi yanayofanya biashara haramu ya dawa za kulevya.


Ziara ya leo itakuwa ni ya kwanza kwa Rais wa Marekani, Latin Amerca na hii ni ziara yake ya pili kubwa nje ya nchi, tangu kushika madaraka, ambapo alifanya ziara ndefu barani Ulaya mapema mwezi huu.


Wakati huohuo wakati Rais Obama akitarajiwa kuwasili nchini Mexico jioni hii,ambapo moja ya masuala atakayozungumzia ni mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, watu kadhaa wameuawa katika mapigano ya kutumia risasi kati ya Wanajeshi na washukiwa wa biashara haramu ya dawa za kulevya.


Tukio hilo limetokea wakati Wanajeshi hao wakifanya doria katika jimbo la kusini la Guerrero, ambapo walijikuta wakishambuliwa na kundi hilo la wahalifu wa dawa za kulevya waliokuwa na silaha, na ndipo wao nao walipojibu mashambulio, miongoni mwa waliouawa ni wanajeshi hao.


Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri. Mohamed Abdul-Rahman