1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Omar al Bashir awasili Sudan Kusini

Mjahida6 Januari 2014

Rais wa Sudan Omar al-Bashir amewasili katika mji mkuu wa Sudan Kusini Juba kwa siku moja ya mazungumzo juu ya mzozo wa nchi hiyo jirani unaoendelea kwa wiki tatu sasa.

https://p.dw.com/p/1AlkH
Salva Kiir und Omar al-Bashir in Khartum 03.09.2013
Rais Salva Kiiir wa Sudan Kusini na mwenzake wa Sudan Omar al BashirPicha: Reuters

Bashir alipokewa katika uwanja wa ndege wa Juba na makamu wa rais wa Sudan Kusini James Wani Igga, alipowasili leo asubuhi kabla ya kuelekea moja kwa moja hadi katika ikulu ya rais kuwa na mazunguzo na rais Salva Kirr.

Bashir hakutoa tamko lolote hadharani wakati wa kuwasili kwake ingawa alipokuwa Khartoum hapo jana aliihakikishia Sudan Kusini kuwa watapata suluhu ya kisiasa ilio na nia ya kuleta amani na kumaliza mgogoro unaoendelea nchini humo.

Kwa upande wake wizara ya mambo ya nchi za nje ya Sudan imesema iko tayari kufanya kila iwezalo katika mamlaka yake kuona juhudi iiowekwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo la mashariki na pembe ya Afrika IGAD katika mgogoro wa Sudan Kusini wa kuwepo kwa mazungumzo na kupatikana kwa amani unafikiwa.

Soldaten in Südsudan
Wanajeshi wa serikali ya Sudan kusiniPicha: picture-alliance/dpa

Mapigano Sudan Kusini yalianza Desemba 15 baada ya rais Salva Kirr kumshutumu Makamu wa rais wa zamani Riek Machar kujaribu kumpindua, madai aliyoyakanusha vikali.

Hatua hiyo ilisababisha mapigano kutoka kwa vikosi vilivyotiifu kwa Machar anayetokea kabila la Nuer na vile vya Salva Kirr kutoka kabila la Dinka.

Mazungumzo yakwama hata kabla ya kuanza Addis Ababa

Sudan Kusini ilijipatia Uhuru wake baada ya kujitenga na Khartoum mwaka wa 2011 lakini bado inaitegemea Sudan kwa kusafirisha mafuta yake.

Huku hayo yakijiri, mazungumzo ya ana kwa ana yanayofanyika mjini Addis Ababa Ethiopia yalikwama hata kabla ya kuanza hapo jana kutokana na serikali ya Sudan Kusini kukataa kuwaachia wafungwa wa kisiasa na matakwa mengine yaliokuwa katika ajenda ya mazungumzo.

Wakati huo huo mapigano yanaendelea kuripotiwa katika maeneo kadhaa nchini Sudan Kusini.

Äthiopien Südsudan Gespräche in Addis Abeba Grang Demebiar
Baadhi ya wajuumbe wa Riek Machar, EthiopiaPicha: Reuters

Hapo jana kulisikika milio ya risasi kwa takriban saa moja nzima katika mji mkuu wa Juba.

Tangu kuanza wa vurugu wiki tatu zilizopita zaidi ya watu 1000 wameuwawa katika taifa hilo jipya na changa duniani huku maelfu wengine wakiachwa bila makaazi.

Wachambuzi wanasema kuna hatari huenda Sudan kusini ikatumbukia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman