1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Sakozy aongoza ujumbe wa Ulaya Moscow

8 Septemba 2008

Urusi yakubali na kuahidi kuzingatia makubaliano ya kusitisha vita

https://p.dw.com/p/FDhT
Rais wa Urusi Medvedev, Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, akiuongoza ujumbe wa Umoja wa Ulaya MoscowPicha: AP

Rais Nikolas Sarkozy wa Ufaransa ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa umoja wa ulaya wa ulaya ameitaka Urusi itekeleze makubaliano ya usimamishaji mapigano, ambayo nchi za magharibi zinasema yanaishurutisha kuondoa majeshi yake katika ardhi ya Georgia. Bw Sarkozy yuko Moscow kwa mazungumzo na viongozi wa Urusi kuhusu mzozo wa Georgia.

Urusi ilizusha lawama kali kutoka nchi za magharibi, ilipopigana vita vya muda mfupi na Georgia mwezi uliopita, ikituma vifaru vaya kijeshi na wanajeshi ndani ya ardhi ya Georgia kulikandamiza jaribio la kuukomboa mkoa wa Ossetia kusini kwa nguvu.

Rais sarkozi alifanikisha kupatikana usiamamishaji mapigano uliomaliza mgogoro huo, lakini serikali za nchi za magharibi zinasema Urusi imekiuka mapatano hayo kwa sababu bado ingali na majeshi yake huko Ossetia kusini na Abkhazia mikoa miwili iliojitenga na ambayo inatambuliwa na nchi hizo kuwa ni sehemu ya ardhi ya Georgia.

Mpaka sasa ni Nicaragua pekee iliojiunga na Urusi kuzitambua Ossetia kusini na Abkhazia kuwa huru.

Rais Sarkozy ambaye anafuatana katika ziara hiyo mjini Mosko na Rais wa halmashauri kuu ya ulaya Jose Manuel Barosso na mkuu wa sera ya kigeni Javier Solana ziara ambayo ni ya pili kufanywa na rais huyo wa Ufaransa tangu mzozo huo kuzuka, katika wadhifa wake kama mwenyekiti wa umoja huo.

Urussi inashikilia kwamba majeshi yake yako katika eneo lililoundwa kama mpaka unaozitenganisha pande zinazohasimiana na kuyazingatia majeshi hayo kuwa ni ya kulinada amani.

Lakini kinyume na matamshi yanayoashiria haja ya kuridhiana na umoja wa ulaya, mvutano na Marekani ulizuaka leo, wakati Russia iliposema inatuma ,anuwari zake ikiwemo inayobeba silaha za nuklea kwa mazoezi katika bahari ya Caribbean, ambapo zitatia nanga nchini Venezuela.

Hatua hiyo inaangaliwa kama ni kulipiza kisasi, baada ya marekani kutuma manuwari kwenye neo la pwani la Georgia zikiwa na shehena ya misaada ya kibinaadamu kwa nchi hiyo, huku Urusi ikidai ni shehena ya silaha.

Umoja wa ulaya wenye wanachama 27 umetishia kusitisha mazungumzo na Urusi kuhusu mkataba mpya wa ushirikiano, ikiwa haitoyaondoa majeshi yake yote nchini Georgia, lakini wadadisi wanasema hilo halitokua na athari kubwa, kwa sababu umoja huo unategemea mafuta na gesi kutoka Urusi.

Akiendelea na juhudi zake za upatanishi kuutatua , Rais Sarkozy anatarajiwa kuzungumza na Rais Dymitry Medvedev juu ya nafasi ya kutumwa

kikosi kipana zaidi cha uwekaji amani Georgia, pendekezo ambalo limetolewa na Urusi, ili iondowe majeshi yake kutoka eneo yaliko hivi sasa.

Wakati huo huo, Shirika moja la habari la Urusi NOVOSTI likimnukuu mwakilishi wa Urusi katika Shirika la kujihami la magharibi NATO akionya kuwa Urusi itavunja uhusiano na shirika la kujihami la magharibi NATO, ikiwa Georgia itapewa uwanachama katika shirika hilo.

Kwa upande mwengine mahakama ya kimataifa mjini The Hague leo imeanza kusikiliza madai ya Georgia kwamba Ursusi ilifanya vitendo vya ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu dhidi ya wenye asili ya Georgia katika maeneo ya Ossetaia kusini na Abkhazia.