1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Sarkozy akutana na Obama

31 Machi 2010

Waitisha vikwazo vikali dhidi ya Iran

https://p.dw.com/p/Mj0Z
Sarkozy na ObamaPicha: AP

Baada ya mazungumzo yake na Rais Barack Obama, Rais Nicholas Sarkozy wa Ufaransa, aliondoka jana usiku Ikulu mjini Washington, kurejea nyumbani pamoja na mkewe Carla Bruni, kufuatia karamu ya usiku.Hakuna maelezo yaliotolewa juu ya mazungumzo yao ya faragha wakati wa karamu hiyo ya muda wa saa 2.

SARKOZY NA OBAMA IKULU

Kufuatia mazungumzo yao ya saa 1 na kitu huko Ikulu, hapo kabla,mjini Washington ,rais wa Ufaransa na wa Marekani,walisimama bega kwa bega wakiitisha kuwekewa haraka vikwazo Iran, juu ya ukaidi wake kwa mradi wake wa nuclear na kuhusu kukomesha mvutano wa miaka mingi baina ya Marekani na Ufaransa.

Rais Sarkozy akiueleza mradi wa nuclear wa Iran ni wazimu mtupu alisema,

"Iran, haiwezi kuendelea na wazimu huu na nimeshamuarifu Obama, kwamba pamoja na Gordon Brown na Angela Merkel tukiwa Ulaya ilioungana, tutazidisha kasi juhudi zetu za kuiiwekea vikwazo Iran."

Nae rais Obama alisema jana mbele ya mgeni wake kwamba,anapendelea vikwazo vipya na vikali vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran na vipitishwe wiki tu zijazo . Hatahivyo, rais Obama, aliungama kuwa kuna dola kuu muhimu ulimwenguni bado hazikuungamkono vikwazo hivyo vipya na vikali.

Rais Sarkozy, alikumbusha kuwa, juhudi za miezi kadhaa za kuiona Iran inaregeza kamba hazikuzaa matunda mema.

G-8

Mbinyo wa pamoja wa marais hao 2 dhidi ya Teheran, uliibuka wakati mawaziri wa nje wa kundi la nchi 8 tajiri (G-8 ) wakikutana nchini Kanada na kudai kwa sauti kali kuwa Iran, ishirikiane na wanachama 5 wa kudumu wa Baraza la Usalama la UM pamoja na Ujerumani.

Waziri wa nje wa Marekani bibi Clinton, alisema kuwa wiki chache zijazo zitajionea mjadala mkali zaidi katika Baraza la Usalama juu ya Iran ambayo nchi za magharibi , zinaitilia shaka inaunda silaha za nuklia. Iran, kwa upande wake,inakataa na kudai inatumia ujuzi wa nuklia kwa nishati.

MASHARIKI YA KATI

Mazungumzo ya jana baina ya rais Sarkozy na Obama, yaligusia pia maswali kadhaa ya kimataifa pamoja na Afghanistan,Mashariki ya Kati na kustawi tena uchumi duniani:

"Tumeafikiana kuendelea kwa juhudi kubwa kudumisha ustawi wa uchumi na kutoa nafasi za kazi kwa watu wetu."

Rais Sarkozy, alisema, ni habari za kupendeza kusikia kuwa, utawala wa rais Obama, umepanga sasa kutanguiliza mbele swali la mageuzi ya mfumo wa fedha.Kwani, mada hii, ilizusha mvutano kati ya Washington na Ulaya huku Marekani, ikionesha haina hamu kubwa ya kuyabana masoko ya fedha ya majambazi kuliko walivyopania viongozi wa ulaya kufanya hivyo.

URAFIKI BINAFSI:

Kuhusu usuhuba kati ya viongozi hao wawili, rais Sarkozy, alimuita rais Obama "rafiki yangu mpenzi" huku akionesha shauku kubwa ya kukomesha kabisa mfarakano wa zamani kati ya Ufaransa na Marekani.

Rais Sarkozy na mkewe , waliondoka jana usiku Washington baada ya karamu yao ya masaa 2 , wakielekea nyumbani Ufaransa kutoka uwanja wa ndege wa kikosi cha wanahewa cha Andrews .

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman