1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Trump kuuhamishia ubalozi wa nchi yake Jerusalem

Oumilkheir Hamidou
6 Desemba 2017

Uamuzi unaotaraajiwa wa rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Jerusalem na uchunguzi wa shirika la IGLU la Ujerumani kuhusu shida za kusoma wanafunzi wengi wa darasa la nne nchini Ujerumani ndio mada kuu magazetini

https://p.dw.com/p/2oq8v
Jerusalem US-Präsident Trump Benjamin Netanjahu
Picha: picture-alliance/Zuma/M. Stern

Tunaanzia njia panda inayoiunganisha Marekani na Mashariki ya kati. Dhamiri ya rais wa Marekani ya kuuhamisha ubalozi wa nchi yake kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem inakosolewa na wahariri wa magazeti takriban yote ya Ujerumani. Wanaonya dhidi ya balaa linaloweza kusababishwa na uamuzi kama huo. Gazeti la  "Rhein-Necker Zeitung la mjini Heidelberg linaandika: "Kuuhamishia ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem na kuutambua mji huo kuwa ndio mji mkuu wa Israel, matokeo yake yatakuwa kuzuka wimbi jengine la ghadhabu za wapalastina-Intifadha. Kwa mara nyengine tena maelfu watapoteza maisha yao. Hilo bila ya shaka halitaishughulisha sana Marekani na pengine  na hata Ulaya pia. Lakini ulimwengu mzima wa kiarabu utatikiswa kwa mapambano ya kikatili ya kuania madaraka. Israel itaendelea kama kawaida kuwa ngome ya utulivu inayofuata maadili ya kidemokrasi. Serikali ya Netanyahu inazongwa na dhana za rushwa na utaratibu wa amani unachujuka."

Uamuzi wa Donald Trump sio wa sadfa

Gazeti la Weser Kurier linasema azma ya rais wa Marekani kuutambua mji wa Jerusalem kua ndio mji mkuu wa Israel si ngeni. Gazeti linaendelea kuandika: "Uamuzi wake wa upande mmoja wa kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, sio wa sadfa.  Tangu katika kampeni zake za uchaguzi Donald Trump alizipigia upatu sera zake  za mashariki ya kati zinazoelemea upande mmoja kwa masilahi ya Israel. Lakini kinachoshitua ni muda aliouchagua. Katika wakati ambapo wapalastina wamekubaliana kuwavua hatamu za uongozi Hamas wanaotajwa kuwa ni magaidi, kiongozi anaetajwa kufuata siasa za wastani Mahmoud Abbas anavunjwa nguvu na pamoja nae ulimwengu wote wa kiislam."

Mtoto mmoja kati ya watano wa darasa la nne hajui kusoma vizuri

 Utafiti wa shirika la IGLU linalochunguza maendeleo ya wanafunzi katika shule za msingi nchini Ujerumani, umebainisha kila mwanafunzi mmoja kati ya watano wa darasa la nne hawezi kusoma vizuri. Gazeti la Schwäbische-Zeitung linaandika: "Haitakuwa sawa kuwatwika jukumu la hali hiyo waalimu wa darasa la nne tu. Hawawezi kufidia makosa yote yanayofanywa na wazee majumbani. Badala ya kuwanunulia watoto vitabu na  vifaa vyenginevyo vya kuelimisha, siku hizi wanachonunuliwa watoto ni komputa za michezo na zana nyenginezo kama hizo. Wataalam wanaonya  kuangalia televisheni kwa muda mrefu, sawa na kucheza na simu za mikono na komputa za mikononi, au tablet sio tu vinapunguza uwezo wa kusoma bali pia watoto hawapati nafasi ya kuyajua mazingira yao na hali hiyo ina madhara pia kwa ubongo wa mtoto. Familia zinabidi zijirekebuishe, zipitishe muda zaidi pamoja na watoto wao."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Mohammed Khelef