1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Afrika Kusini aelekea Japan leo huku akiacha mzozo nyumbani

Mwakideu, Alex27 Mei 2008

Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki amewasili nchini Japan kwa kongamano la kujadili maendeleo ya Afrika huku akiwacha ghasia za kuwafukuza raia wa kigeni zikiendelea nchini mwake.

https://p.dw.com/p/E720
Rais wa Afrika Kusini Thabo MbekiPicha: AP

Rais Mbeki amekuwa akishutumiwa kwa utaratibu wake wa kuzuia ghasia hizo.


Rais huyo anahudhuria kongamano la nchi arobaini za Afrika linalojadiliana njia za kupunguza umaskini, upungufu wa chakula duniani na maendeleo ya Afrika huku mashirika ya misaada yakionya kwamba ghasia zinazowakabili raia wa kigeni Afrika Kusini zinaendelea kupamba moto.


Kabla ya kupanda ndege kuelekea nchini Japan Rais Mbeki aliambia waandishi wa habari kwamba pamoja na yote yatakayojadiliwa nchini humo ataitumia ziara yake kuendeleza uhusiano wa Afrika Kusini na Japan akilenga kuimarisha zaidi maeneo ya kaskazini na Kusini.


Lakini licha ya hayo Rais huyo amekuwa akishutumiwa kwa kutoshughulikia vyema ghasia zinaoikabili nchi yake ambapo raia wa kigeni wanavamiwa na kuuwawa na mali zao zinaharibiwa.


Mashirika ya misaada yametoa onyo la kuzuka kwa magonjwa na kupungua kwa misaada wakati idadi ya walioachwa bila makao ikizidi watu 35 elfu na waliouawa katika ghasia hizo ikitimia watu 56.


Nchi jirani ya Msumbiji imeripoti kurejea nyumbani kwa raia wake elfu ishirini na sita huku Malawi ikipanga kuwaondoa raia wake elfu tatu nchini Afrika Kusini.


Wakati huo huo shirika la msalaba mwekundu linasema limejiandaa kuwapokea wakimbizi 25 elfu raia wa Zimbabwe nchini Zambia.


Wakati maelfu ya raia wa kigeni wanakimbilia mipakani hali mbaya ya kibinadamu inaikabili Afrika kusini kwani takriban wakimbizi 35 elfu wanajistiri katika vituo vya polisi, vya kijamii na makanisa.

Rais Thabo Mbeki ambaye alitoa wito wa amani hapo mwishoni mwa wiki anaongoza jopo maalum la mawaziri 11 lililoundwa kwa ajili ya kukabiliana na ghasia hizo "Aibu, Aibu, Aibu inayodhalilisha nchi yetu, ambapo kuna watu kidogo tu, wachache katika jamii zetu wanaoamua kutekeleza uhalifu dhidi ya waafrika wenzao” Mbeki alisema.


Raia wa kigeni nchini Afrika Kusini wengi wao kutoka nchi jirani ya Zimbabwe wanalaumiwa kwa uhalifu na pia kupata nafasi za kazi ilhali raia wenyewe hawana nafasi hizo.


Makundi ya vijana yanaripotiwa kuvamia vitongoji duni vilivyoko katika viunga vya mji wa Johannesburg. Hadi sasa ugogoro huo wa kuwafukuza raia wa kigeni umesambaa katika mikoa tisa tangu ulipoanza tarehe 11 mwezi huu.


Akihojiwa na wanahabari mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete alisema "naweza kusema hadi kufikia sasa habari za chuki dhidi ya wageni nafikiri zitakuwa za kuongeza chumvi. Kama ingekuwa kitu kinachowahusu raia wote wa Afrika Kusini………lakini unaona ni kisa cha kipekee kinachoendeshwa na makundi fulani ambayo tayari serikali ishayatambua."


Wakati ghasia hizo zinaendelea kuiletea hasara Afrika Kusini shirika la msalaba mwekundu limelalamika kwamba hakuna ushirikiano wa kitaifa.


Mkurugenzi wa shirika hilo kusini mwa Afrika Francoise Le Goff amesema usambazaji wa habari kutoka kwa serikali hadi kwa mashirika yasiokuwa ya kiserikali hauendelei vizuri.


Shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka limeambia AFP kwamba hali nchini Afrika Kusini inaelekea kuwa mbaya zaidi kwani kuna watu ambao bado hawajapokea misaada na hawana hata mahema ya kuishi.


Wadadisi wanasema nchi hiyo inakabiliwa na matatizo kwasababu haijazingatia mikakati ya kutatua maswala ya upungufu wa nyumba, ongezeko la raia wa kigeni, na hali ya umaskini katika vitongoji duni vilivyoko katika viunga vya miji mikuu nchini humo.


Licha ya hali kuonekana kuwa tulivu hapo jana baada ya msako mkali ulioendeshwa na maafisa wa polisi, ghasia ziliripotiwa katika maeneo machache na wasi wasi ungali umetanda nchini humo.