1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Benki ya dunia Paul Wolfowitz asema anatumai wafaadhili watatoa fedha zaidi kwa ajili ya nchi masikini.

Mohammed Abdul-Rahman2 Machi 2007

Rais wa Benki ya dunia Paul Wolfowitz anatumai kwamba Marekani itakua Kiongozi na sio dola inayofuata maamuzi tu, panapohusika na suala la utoaji mpya wa fedha kwa nchi masikini duniani, wakati wa majadiliano baina ya wachangiaji w40 wakubwa katika benki hiyo, utakaoanza mjini Paris wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/CHJ1
Rais wa Benki ya dunia Paul Wolfowitz.
Rais wa Benki ya dunia Paul Wolfowitz.Picha: AP

Katika mahojiano na Shirika la habari la Reuters, kabla ya ziara yake katika nchi nne za Afrika inayoanza leo Ijumaa, Bw Wolfowitz alisema anatarajia fedha mpya kutoka kwa nchi zinazotokeza sasa kama wakopeshaji ,mfano zile tajiri zinazotoa mafuta.

Benki ya dunia hushughulikia masuala ya mikopo kupitia wakala wa maendeleo wa kimataifa, International Development Agency-IDA, ambao ni mkopeshaji mkubwa duniani kwa nchi masikini.

Sehemu kubwa ya kiasi cha dola 9.1 bilioni kila mwaka kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hutolewa kwa mataifa ya Afrika na kusini mwa Asia zikiwemo India, Afghanistan na Pakistan.

Safari hii majadiliano hayo ya wafadhili wakubwa mjini Paris, huenda yakawa magumu, kutokana na hatua za kufunga mkaja takriban kote katika nchi tajiri duniani, pamoja na kujitolea zaidi kwa mfadhili mkubwa , Marekani, katika vita dhidi ya ugaidi vinavyoigharimu kitita kikubwa cha fedha.

Wakala wa maendeleo wa IDA, una mahitaji ya fedha za kutosha ,hasa baada ya kundi la mataifa manane yalioendelea kiviwanda G8, kukubali mwaka 2005 kuyafutia mzigo wa madeni mataifa 19 miongoni mwa wakopaji masikini wakubwa kutoka Benki ya dunia, jambo ambalo linaweza kuzusha ukosefu wa fedha katika wakala huo wa maendeleo, ikiwa wafadhili watashindwa kutekeleza ahadi zao za kuongeza fedha zao.

Kuwa na wakala mdogo wa maendeleo wa kimataifa, kutakua na maana fedha kidogo zaidi kwa nchi masikini na hali hiyo itapunguza pia mfuko wa fedha kwa wakopaji wapya. Mnamo mwaka 2005, wafadhili waliahidi michango mipya ya jumla ya dola 18 bilioni.

Rais wa Benki ya dunia Wolfowitz anasema,anachotarajia ni kwamba baadhi ya wafadhili ambao michango yao imekua ikipungua, sasa watachangia zaidi, ikiwa ni pamoja na Marekani.

Marekani na wafadhili wengine, wamezusha wasi wasi wao kwamba nchi za kiafrika zilizofutiwa madeni, zinaweza zikawa zinachukua mzigo mwengine kutokana na kuzuka kwa mikopo mipya kutoka nchini kadhaa zikiwemo China na India.

Waakilishi wa nchi fadhili mjini Washington-makao makuu ya Benki ya dunia, wanasema Bw Wolfowitz binafsi ambaye alikua waziri mdogo wa ulinzi wa Marekani kabla ya kushika wadhifa huo wa kuiongoza hiyo, atakua mtu muhimu katika kuwashawishi wafadhili na kiasi cha fedha zaidi watakachokua tayari kuchangia. Baadhi yao wameshazozana na Bw Wolfowitz katika masuala kama vile msimamo wa benki ya dunia katika kupambana na rushwa. Lakini rais huyo wa benki ya dunia anasema litakua kosa na ni kuziadhibu nchi masikini, iwapo maamuzi ya wafadhili yatakua ni kwa sababu ya tafauti zao na yeye.

Pamoja na hayo ameeleza kwamba baadhi ya mataifa wafadhili yameelezea nia ya kuwa tayari kuyaasaidia mataifa yaliotajwa kuwa katika hali tete, ambayo ni pamoja na yale yaliyotoka katika migogoro na vita kama Liberia, Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo au Afghanistan, wakati ambapo wafadhili wengine wanashinikiza juu ya utoaji fedha zaidi, kwa ajili ya miradi ya miundo mbinu katika kanda mbali mbali ikiwa ni pamoja na barani Afrika.