1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Gabon atangaza kugombea tena urais

Mjahida29 Februari 2016

Rais Ali Bongo Ondimba, ambaye babake aliitawala Gabon kwa miaka 41, amesema atawania muhula mwengine wa pili wa rais katika nchi hiyo tajiri kwa mafuta, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

https://p.dw.com/p/1I4NX
Ali Bongo Ondimba, neuer Präsident von Gabun
Rais wa Gabon,Ali Bongo Ondimba,Picha: AP

Akizungumza katika eneo la mashambani la Ozouri, ambapo mafuta yalipatikana kwa mara ya kwanza mwaka wa 1950, Rais Bongo alisema anatangaza wazi kugombea tena katika uchaguzi huo wa rais unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti japokuwa bado tarehe rasmi haijawekwa wazi.

Iwapo atachaguliwa tena, Rais Ali Bongo ameapa kupambana na masuala ya upendeleo na kujenga maisha yaliyo bora zaidi kwa raia wake. Watu milioni 1.6 wanaoishi nchini humo wengi wao ni masikini licha ya taifa hilo kuwa tajiri kwa mafuta. Bongo pia ameahidi kufufua vyanzo mbali mbali vya uchumi katika taifa hilo ambalo mafuta yanachangia asilimia 60 ya uchumi wa nchi.

Wahlen in Gabun 2009
Raia wa Gabon wakati wa uchaguzi mwaka wa 2009, uliyompa ushindi rais BongoPicha: AP

Ali Bongo aliingia madarakani baada ya kufanyika uchaguzi uliyokuwa na utata mwaka wa 2009 kufuatia kifo cha babaake Omar Bongo Ondimba, aliyeiongoza Gabon tangu mwaka wa 1967 ambaye wakoasoaji wamemueleza kama mtu aliyekuwa mfisadi.

Kwa sasa anaelekea kumaliza muhula wake wa miaka saba madarakani. Hakuna kikomo cha madaraka kwa rais nchini Gabon.

Aidha viongozi wengine wa Afrika wamekuwa na tabia ya kuongeza mihula yao madarakani huku wengine wakibadilisha katiba ili kufanya hivyo kama Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Congo ambapo mapigano makali yametokea.

Hivi maajuzi rais wa Gambia Yahya Jammeh alipitishwa na chama chake kuwania muhula wa tano madarakani katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Utata waibuka juu ya cheti cha kuzaliwa cha rais Ali Bongo

Huku hayo yakiarifiwa makakama moja katika mji mmoja wa kifaransa wa Nantes imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na dadake wa kambo rais Ali Bongo inayodai cheti cha kuzaliwa cha rais huyo ni cha kughushi.

Hata hivyo wakati uchaguzi ukikaribia nchini Gabon kumekuwa na utata juu ya mahali alikozaliwa rais huyo huku wakosoaji wakisema amebadilisha cheti chake cha kuzaliwa kuficha ukweli kwamba alichukuliwa kutoka nchi nyengine.

Ali Bongo Ondimba, neuer Präsident von Gabun
Rais wa Gabon,Ali Bongo Ondimba,Picha: AP

Kulingana na katiba ya Gabon, kiongozi wa nchi anapaswa kuwa raia aliyezaliwa nchini humo. Lakini mwaandishi habari wa ufaransa Pierre Pean alidai katika kitabu vhake kwamba rais Ali Bongo ni raia wa Nigeria, na alichukuliwa na kulelewa Gabon wakati wa vita vya Biafran mwishoni mwa mwaka 60.

Mwenyewe Rais Bongo anadai kuzaliwa Brazzaville mwaka 1959. Taasisi ya usajili ya Nantes ndio inayoshughulikia vyeti vyote vya kuzaliwa vya watu waliyozaliwa katika nchi zilizotawaliwa na Ufaransa hadi mwaka wa 1960, ambapo nchi zilizokuwa koloni katika eneo hilo zilipata uhuru na kuwa Gabon Congo, Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwandishi: Amina AbubakarAFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef