1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Iran asema Marekani inahusika na shambulio la Septemba 11

24 Septemba 2010

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, amesema kuwa watu wengi wanaamini kuwa serikali ya Marekani ndiyo iliyoandaa shambulio la kigaidi la Septemba 11 katika kituo cha biashara cha kimataifa jijini New York.

https://p.dw.com/p/PLgd
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran akihutubia Umoja wa MataifaPicha: AP

Kauli yake hiyo, ambayo aliitoa wakati alipokihutbia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ilisababisha wajumbe kutoka mataifa ya magharibi kutoka nje ya ukumbi kunakofanyika mkutano huo, ambao uko umbali wa kiasi cha kilomita sita kutoka kwenye eneo lilikofanyika shambulio hilo.

Rais Ahmednejad, ambaye alihutubia muda mfupi baada ya Rais Barack Obama kuhutubia kikao hicho na kuendelea kunyoosha mkono wa kutaka kuzungumza na Iran, kuhusiana na mpango wake wa nyuklia, alisema kuwa kuna dhana iliyopo inayoonesha kuwa serikali ya Marekani iliandaa shambulio hilo, kwa manufaa yake na wale aliyowaita watawala wa kizayuni.

´´Kuna ishara kwamba serikali ya Marekani iliandaa shambulio hilo, ili kutumia nafasi hiyo kuufufua uchumi wake uliyokuwa umeyumba, na pia kuzidisha ushawishi wake katika eneo la mashariki ya kati. Hayo yote ni katika kuusaidia utawala wa kizayuni´´

´

Ameongeza kuwa idadi kubwa ya wananchi wa Marekani pamoja na wale wa mataifa mengine halikadhalika na wanasiasa wanakubaliana na mtizamo huo.

Katika shambulio hilo lililotokea mwaka 2001, takriban watu elfu tatu walikufa baada ya magaidi wa kundi la mtandao wa Al-Qaida kuziteka ndege na kuzibamiza katika jengo la kituo cha biashara cha kimataifa, WTC. Ndege nyingine ziliangukia katika makao makuu ya wizara ya ulinzi, Pentagon, na nyingine Pennsylvania.

Kauli hiyo Rais wa Iran imelaaniwa na mataifa ya magharibi ambapo mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Bibi Catherine Ashton, amesema ni kauli ya kufedhehesha na isiyokubalika.

Mapema Rais Obama, katika hotuba yake kabla ya Rais Ahmednejad kuhutubia, aliionyoshea mkono wa mazungumzo nchi hiyo kuhusiana na mpango wake wa nyuklia wenye utata.

UN Obama Rede Generalversammlung
Rais Barack ObamaPicha: AP

´´Marekani na Jumuiya ya kimataifa inatafuta suluhisho la tofauti zetu na Iran, na mlango bado uko wazi iwapo Iran itakubaliana kuingia katika kutatua tatizo hili kwa njia ya kidiplomasia´´

Lakini kwa upande wake, Rais Ahmednejad akizungumzia suala hilo , aliyashutumu mataifa yenye nguvu duniani kwa kujaribu kuizuia kutumia nishati ya nyuklia, na kwamba yanataka kuhodhi matumizi ya nishati hiyo huku yakizidi kuimarisha silaha zao za nyuklia.

´´Iran mara zote imekuwa tayari kuingia katika majadiliano, lakini yatakayozingatia kuheshimiana na ya haki. Wale wote wanaotumia vitisho na vikwazo dhidi ya haki iliyo wazi ya taifa la Iran, kwa kweli wanaiharibu sifa na hadhi iliyosalia ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa´´

Mjini Tehran, shirika la habari la Iran limemnukuu Rais Ahmednejad akisema kuwa huenda nchi hiyo ikaanza majadiliano na mataifa yenye nguvu duniani mwezi ujayo kuhusiana na mpango wake huo.

Mapema Waziri wa nje wa Marekani, Bibi Hillary Clinton, na wenzake wa Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, China na Urusi walitoa wito wa kuanza haraka majadiliano na Iran.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/AFP/ZPR

Mhariri:Othman Miraji