1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Iran katika chuo kikuu cha Columbia New-York

Oummilkheir25 Septemba 2007

Ahmadinedjad hajali matusi ya mkuu wa chuo kikuu cha Columbia dhidi yake.

https://p.dw.com/p/CH7m
Rais wa Iran
Rais wa IranPicha: AP

Rais Mahmoud Ahmadinedjad amekaripiwa hadharani katika chuo kikuu cha Columbia mjini New-York na kuitwa “muimla habithi na muovu” na mkuu wa chuo kikuu hicho Lee Bollinger.

Hotuba ya kiongozi huyo wa Iran katika chuo kikuu cha Columbia,iliyojiri siku moja kabla ya kuhutubia baraza kuu la umoja wa mataifa,ilizongwa na vuta nikuvute iliyopaliliwa na vyombo vya habari na baadhi ya wanasiasa pia.

Akizomewa na wengi na wengine kumshangiria,na kukumbushwa hoja alizowahi kuzitoa kuhusu mauwaji ya halaiki ya wayahudi wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia-Holocaust au hoja zake dhidi ya Israel,Mahmoud Ahmadinedjad alifanya kana kwamba hayakamushughulisha yaliyosemwa.Lakini alilalamika baadae dhidi ya “matamshi ya kuchukiza” ya Lee Bollinger.

Rais huyo wa Iran aliutumia mjadala huo kuzisuta lawama dhidi yake na hasa pale aliposhuku kama mauwaji ya halaiki ya wayahudi-Holocaust yaliwahi kutokea na kutetea pia haki ya jamhuri ya kiislam ya Iran kuendelea na mpango wake wa kinuklea kwa matumizi ya amani.Amesisitiza kwa mara nyengine tena Iran haina azma ya kutengeneza silaha za kinuklea.

Lakini hata kabla ya kuanza kuhutubia,rais huyo wa Iran alikaripiwa kwa dakika kumi nzima na mkurugenzi mkuu wa chuo kikuu cha Columbia Lee Bollinger: “Bwana rais,unaonyesha kila ishara ya kua kijiimla kidogo na habithi.”

Amesema hayo bwana Bollinger akimlaumu kiongozi huyo wa Iran kwa kuwakandamiza wasomi na walawiti.

“Kwanini umeingiwa na woga kuwaona wairan wakitoa maoni yao?-amemuuliza.Siamini kama una moyo wa mtu mwenye kipaji kuweza kujibu masuala haya” ameongeza kusema mkuu huyo wa chuo kikuu cha Columbia.

“Unapokuja katika mahala kama hapa unajitia aibu tuu.Ama wewe ni mchokozi,au hukupata malezi “ameendelea kusema Lee Bollinger.

Aliponyanyuka kuhutubia,Mahmoud Ahmedinedjad,amemlaumu Bollinger kwa “kumtukana na kumsingizia.”

Akionekana kama kwamba matusi dhidi yake hayamsumbuwi,rais Mahmoud Ahmadinedjad amezungumzia haki ya Iran ya kuendelea na mradi wake wa kinuklea na vizingiti vinavyowekwa na Marekani katika kulifikia lengo lake.

“Hatuthamini silaha za kinuklea”-amesema.

Akitabasamu na hata kuchekelea,rais Ahmadinedjad amezungumzia utamaduni wa Iran na matumaini yao.Alizomewa alipodai kwamba nchini Iran hakuna mashoga.

Rais Ahmadinedjad anasema:“Hatuna mashoga nchini Iran,kiroja hicho hakipo sijui mmezipata wapi habari hizo“.

Akiulizwa kuhusu mauwaji ya halaiki ya wayahudi katika vita vikuu vya pili vya dunia,rais Mahmoud Ahmadinedjad amesema tunanukuu:“ sisemi kama hayajatokea,nasema uchunguzi ziada unahitajika.“mwisho wa kumnukuu.

Nje ya chuo kikuu hicho dazeni kadhaa ya waandamanaji walibeba mabango yenye maandishi „Mkamateni Ahmedinedjan,Hitler wa Iran.“

Maombi ya Ahmadinedjad ya kutembelea “ Ground Zero“-kulikokuwepo zamani jengo la World Trade Center,yamekataliwa,opolisi ikitoa sababu za usalama.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleeza Rice amesema“ maombi hayo ni kiini macho tuu.“