1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto apongeza azimio la Baraza la Usalama la UN kuhusu Haiti

Tatu Karema
4 Oktoba 2023

Rais William Ruto wa Kenya leo amelipongeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kupitisha azimio la kutuma jeshi la kimataifa linaloongozwa na Kenya nchini Haiti kukabiliana na magenge ya uhalifu.

https://p.dw.com/p/4X4kd
Afisa wa zamani wa polisi Jimmy "Barbecue" Cherizier, kiongozi wa muungano wa 'G9', anaongoza maandamano dhidi ya waziri mkuu wa Haiti Ariel Henry akizingirwa na maafisa wake wa usalama mjini Port- au- Prince mnamo Septemba 19, 2023
Afisa wa zamani wa polisi Jimmy "Barbecue" Cherizier, kiongozi wa muungano wa 'G9', anaongoza maandamano dhidi ya waziri mkuu wa Haiti Ariel Henry akizingirwa na maafisa wake wa usalama Picha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Kauli ya Ruto inajiri masaa machache baada ya kura ya Jumatatu katika baraza hilo la Umoja wa Mataifa, hii ikiwa ni mara ya kwanza katika muda wa takribani miaka 20 kwa wanajeshi kutumwa nchini Haiti ambako magenge ya uhalifu yamekuwa yakifanya mauaji, utekaji nyara na ubakaji.

Soma pia:Jeshi la polisi nchini Haiti limeelemewa na wingi wa magenge na uhalifu unaofanywa na magenge hayo

Ruto amesema kikosi hicho kitakachoongozwa na Kenya, kitatoa mwelekeo tofauti katika historia ya uingiliaji kati wa vikosi vya kimataifa nchini Haiti:

Kikosi cha kimataifa kupelekwa Haiti kwa muda wa mwaka mmoja

Azimio hilo, ambayo rasimu yake iliandikwa na Marekani na Ecuador, linaidhinisha kikosi hicho kupelekwa nchini humo kwa muda wa mwaka mmoja, na baada ya miezi tisa ya kufanyiwa tathmini.

Kikosi ambacho hakitakuwa cha Umoja wa Mataifa pkitafadhiliwa kwa michango ya hiari huku Marekani ikiahidi hadi dola milioni 200.

Haikubainishwa mara moja ukubwa wa kikosi hicho kitakachopelekwa Haiti, ingawa awali serikali ya Kenya ilikuwa imependekeza maafisa wa polisi 1,000.

Rais Ruto hakubainisha wakati watakaposafiri, lakini waziri wa wake wa mambo ya nje, Alfred Mutua, jana usiku alisema hilo litafanyika ndani ya muda mfupi.

Soma pia:Umoja wa Mataifa wasema ghasia za magenge ya wahalifu zaongezeka nchini Haiti

Awali, Mutua alikuwa amesema kuwa Kenya ilikuwa inasubiri matokeo ya kura ya Baraza la Usalama lakini mipango inaendelea na kwamba maafisa wakuu wa Kenya wameanza kujifunza lugha ya Kifaransa ili kuepuka hali ya kutoelewana kilugha kati yao na Wahaiti.

Mkuu wa polisi Kenya aelezea matumaini ya ufanisi wa ujumbe wa amani

Rais wa Kenya William Ruto akihutubia wakati wa ufunguzi wa kongamano la Afrika la hali ya hewa mjini Nairobi mnamo Septemba 4, 2023
Rais wa Kenya William RutoPicha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Siku ya Ijumaa, mkuu wa polisi nchini Kenya, Japhet Koome, alielezea matumaini kwamba ujumbe huo wa amani utafanikiwa.

Hata hivyo, maafisa wa polisi wa Kenya kwa muda mrefu wameshtumiwa na mashirika yanayofuatilia masuala ya rushwa kwa matumizi mabaya ya nguvu, mateso na unyanyasaji mwingine.

Afisa wa zamani wa polisi anayechukuliwa na wengi kuwa kiongozi mwenye ushawishi zaidi wa magenge nchini Haiti, Jimmy Cherizier, almaarufu Barbacue, ameonya kwamba atapambana na kikosi chochote cha kimataifa kitakachopelekwa nchini humo iwapo kitajihusisha katika unyanyasaji wa aina yoyote.

Soma pia: Magenge yenye silaha nchini Haiti yataka serikali ipinduliwe

Kenya ilijitolea kuongoza ujumbe huo wa Haiti, ikitaja historia yake katika misheni za amani ulimwenguni pamoja na uhusiano kati ya Afrika na Haiti, ambayo watu wake wengi wana asili ya Kiafrika.

Kura hiyo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imefanyika karibu mwaka mmoja baada ya serikali ya Haiti kuomba kutumwa mara moja kwa kikosi cha kimataifa kukabiliana na ongezeko la magenge ya uhalifu na kurejesha usalama nchini humo, ili kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu.