1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Maldives ajiuzulu

7 Februari 2012

Rais wa visiwa vya Maldives, Mohamed Nasheed, amejiuzulu hii leo (07.02.2012) baada ya vikosi vya polisi kuanzisha uasi kufuatia wiki tatu za maandamano ya upinzani unaodai kuachiwa huru rais wa mahakama ya jinai.

https://p.dw.com/p/13yPv
Rais Mohammed Nasheed wa Maldives
Rais Mohammed Nasheed wa MaldivesPicha: dapd

Rais Mohammed Nasheed ametangaza uamuzi wake wa kujiuzulu wakati wa mkutano na waandishi habari, kupitia televisheni ya taifa hii leo.

"Itakuwa vyema kwa nchi, katika hali ya sasa, ikiwa nitajiuzulu.Sitaki kutawala kwa mkono wa chuma. Nnajiuzulu-amesema rais Mohamed Nasheed aliyemkabidhi madaraka makamo wa rais, Mohamed Waheed Hassan Manik,

Hapo awali, duru kutoka ikulu ya rais zilisema rais "hana azma ya kujizulu."

Vikosi vilivyoasi vya polisi vililidhibiti jengo la televisheni ya taifa na kuanza kutoa miito kutaka rais apinduliwe.

Visiwa hivyo vya bahari ya Hindi vinavyopendwa sana na watalii kutokana na fukwe zake za kuvutia, vimetumbukia katika mzozo wa kisiasa tangu alipokamatwa kwa tuhuma za kuhusika na rushwa rais wa korti kuu ya jinai, Abdullah Mohammed, kati kati ya mwezi uliopita. Madai ya korti kuu na mwanasheria mkuu kutaka aachiliwe huru hayakuitikwa.

Tangu wakati huo, wafuasi wa upande wa upinzani wamekuwa wakiteremka majiani kudai rais Nasheed, mwanaharakati wa zamani wa haki za binaadam,ajiuzulu, wakifika hadi ya kumtuhumu anataka kuiongoza nchi hiyo kimabavu.

Wanajeshi wa Maldives
Wanajeshi wa MaldivesPicha: dapd

Chama cha upinzani cha kiongozi wa zamani wa Maldives, Maumoon Abdul Gayoom, kinawalaumu wanajeshi kufyetua risasi za mpira dhidi ya waandamanaji, na msemaji wa chama hicho, Mohammesd Hussain "Mundhu" Shareef, alisema "watu kadhaa wamejeruhiwa."Hakutoa lakini idadi halisi.

Maafisa wa serikali walikanusha madai hayo, lakini walithibitisha ripoti kwamba maafisa kama 30 wamekataa kutii amri na kuyavamia makao makuu ya chama tawala.

Maandamano hayo yanayoizonga nchi hiyo katika wakati ambapo inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwakani, yamechukua sura ya itikadi kali, huku rais aliyejiuzulu, Mohamed Nasheed, akituhumiwa kupinga dini ya kiislam.

Maandamano ya upinzani mjini Male - mji mkuu wa Maldives
Maandamano ya upinzani mjini Male - mji mkuu wa MaldivesPicha: dapd

Machafuko haya yanatoa sura pia ya uhasama wa muda mrefu unaoendelea kati ya Maumoon Gayoom na Nasheed aliyewahi kukamatwa mara 27 wakati wa utawala wa miaka 30 wa mtangulizi wake.

Mohammed Nasheed, mwanaharakati wa haki za binaadamu, ni kiongozi wa kwanza kuingia madarakani kufuatia uchaguzi wa vyama vinyi vya kisiasa mnamo mwaka 2008 katika visiwa hivyo vya bahari ya Hindi.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Miraji Othman