1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Marekani atapatapa mithili ya mfa maji

5 Juni 2007

Hali inayoendelea kuzorota nchini Irak, upinzani wa chama cha Demokratik na mtazamo tafauti wa baadhi ya washirika wakuu wa Marekani katika maswala mbali mbali huenda yakachangia kumlainisha rais George Bush na kumalzimu ashirikiane na wenzake katika mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la nchi nane zilizostawi kiviwanda G8 katika mji wa Heiligindamm kaskazini mwa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHDB
Rais George W Bush wa Marekani
Rais George W Bush wa MarekaniPicha: AP

Bila shaka rais George W Bush wa Marekani ameshtukia hali tete inayomkabili na kwa ajili hiyo amezindua mikakati mbali mbali pamoja na mazungumzo ya awali kabla ya mjadala na viongozi wa nchi nane zenye nguvu ulimwenguni.

Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema kwa kufanya hivyo rais Bush anajaribu kuiremba sura ya Marekani na kufunikiza msimamo wake usiokuwa na uhai kwa ulimwengu.

Katika hotuba yake kabla ya mkutano wa kilele mjini Heiligendamm hapa nchini Ujeurmani rais Bush ametangaza ongezeko la mchango wa Marekani katika kupambana na maradhi ya Ukimwi kufikia dola bilioni 30 kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2013, pia amelitaka bunge la Kongress kuidhinisha ongezeko la misaada kwa bara la Afrika hadi dola bilioni 8.67 kufikia mwaka 2010.

Bush ambae alizama katika maswala ya vita vya Irak katika awamu mbili za utawala wake, ametangaza azma yake ya kutaka kuzuru nchi zinazokabiliwa na umasikini mkubwa barani Afrika zikiwa ni pamoja na Senegal, Msumbiji, Zambia na Mali ili kujionea mwenyewe kwa macho yake.

Rais Bush ambae amelaumiwa mara kwa mara na makundi ya wanaharakati kwa kutofanya jitihada zaidi kuzuia maafa ya kibinadamu katika jimbo la Darfur nchini Sudan amezindua vikwazo mbali mbali kuwalenga wakuu wa utawala wa Sudan wanaotuhumiwa kuhusika na mashambulio yaliyosababaisha vifo vya takriban watu laki nne.

Mbali na mikakati kadhaa iliyotangazwa na rais Bush swala lililo zusha utata ni swala la mpango wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Marekani ikiwa ndio taifa kubwa linalo ongoza kiuchumi na mchafuzi mkubwa wa mazingira duniani imependekeza mfumo mpya wa makubaliano ya kimataifa wa kupambana na gesi chafu zinazotoka viwandani utakao tumika badala ya itifaki ya Kyoto ya mwaka 1997 ambayo Marekani imegoma kutia saini kwa hofu kuwa mkataba huo utaiwekea nchi yake vipingamizi vya kiuchumi na maendeleo.

Mfumo huo mpya wa rais Bush unalenga nchi 10 hadi 15 ambazo zinamatumizi makubwa ya nishati na zinatoa gesi chafu kwa kiwango kikubwa pia rais Bush amesema atawahimiza viongozi wengine waongeze uwekezaji katika utafiti wa nishati mbadala ili kupunguza kutegemea mafuta zaidi.

Mapendekezo hayo huenda yakamsaidia Bush kupata pa kuegemeza kichwa kutokana na kuungwa mkono na baadhi ya nchi kwani nyumbani kwake baadhi ya viongozi wameukosoa utawala wake hasa katika maswala yanayohusisha pande nyingi.

Vile vile Bush atakabiliwa na changamoto ya kuboresha uhusiano na Ufaransa ambao ulizorota wakati wa utawala wa rais mstaafu Jacque Chirac kutokana na hatua ya Marekani ya kuivamia Irak.

Hii pia itakuwa ni mara ya mwisho kuhudhuria mkutano huu wa kilele kwa rafiki mkuu wa rais Bush barani Ulaya waziri mkuu wa Uingereza anayeondokaza Tony Blair.