1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

120710 Johnathan Facebook

Josephat Nyiro Charo12 Julai 2010

Siasa kwenye mtandao wa mawasiliano wa intaneti! Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amejiunga na viongozi wengine mashuhuri ulimwenguni kutumia tovuti ya kijamii ya facebook kuwasiliana na kujadiliana na wananchi wake

https://p.dw.com/p/OHQV
Rais wa Nigeria Jonathan GoodluckPicha: AP

Katika taifa linalokabiliwa na migawanyiko ya kikabilia na kidini, hatua hii inampa fursa kiongozi huyo kutoa maoni yake kuhusu masuala mbalimbali nchini Nigeria. Kwa Wanigeria wengi, kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na rais wao kwenye facebook, ni jambo geni kabisa! Je Wanigeria wanaipokeaje hatua hiyo ya rais wao?

Kwa rais wa Marekani Barack Obama na kansela wa Ujeruamni Angela Merkel, tovuti ya kijamii ya facebook, imekuwa chombo muhimu cha mawasiliano na umma. Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu zaidi ya watumiaji wa facebook milioni 400 duniani walipata mgeni - rais wa Nigeria Goodluck Jonathan.

Shauku ya nafasi hii mpya kutoka ikulu ya mjini Abuja ni kubwa mno. Ukurasa wa rais kwenye tovuti ya facebook ulikuwa haujatimiza wiki mbili na tayari watu zaidi ya 100,000 walikuwa wameutembelea na kujiandikisha ili kujisomea anachokiandika rais Jonathan. Kwa kulinganisha, ukurasa wa kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ambao sasa umekuwa ni wa tangu zamani, mpaka sasa una wanachama 40,000 tu. Hata hivyo rais Jonathan hajamfikia rais wa Marekani, Barack Obama, ambaye ukurasa wake wa facebook una watumiaji zaidi ya milioni 10 waliojiandikisha.

Kwenye facebook watumiaji wa mtandao wa intaneti wanaweza kujisajili na kuandika taarifa zao na hata kuweka picha. Watumiaji wengine wanaweza kuzisoma taarifa hizo na kuandika maoni yao au kuweka alama kama wamependwa na ukurasa fulani. Halafu wanahesabiwa kama mashabiki wa ukurasa huo na kujulishwa kuhusu taarifa mpya za ukurasa huo kwenye ukurasa wao binafsi.

Katika mkahawa wa mtandao wa intaneti mjini Sokoto, kaskazini magharibi mwa Nigeria, mwanamke huyu tayari ameufungua ukurasa wa rais wa Goodluck Jonathan.

"Hayo ni maendeleo mapya ambayo lakini ni mazuri. Anawapa Wanigeria wote nafasi ya kuwaambia wanasiasa moja kwa moja kuhusu maoni yao. Kama kuna mapungufu, mambo yanaweza kurekebishwa. Mbali na rais, kuna wanasiasa wengine ambao tayari wamo kwenye facebook. Wanatoa maoni yao kuhusu mada mbalimbali kama sisi, bila kuwa na hofu ya kukamatwa. Uwezekano huu unapunguza pengo kubwa lililopo kati ya wanasiasa na wananchi."

Kufikia sasa Wanigeria milioni moja wamejisajili kwenye facebook. Idadi hii inaufanya mtandao huu wa kijamii kuwa na mvuto mkubwa kwa wanasiasa. Wanauona kama nafasi nzuri ya kujadiliana na wananchi wao, kuyasikilza maoni na matatizo yao ili kwa pamoja kuweza kutafuta suluhisho lifaalo.

Yakubu Musa, ambaye ni afisa anayehusika na kazi za nje za rais Jonathan, anasema siku ya kwanza ya kufungua ukurasa wa rais kwenye facebook ilikuwa ya ufanisi mkubwa. Hata hivyo anasema yeye haruhusiwi kuandika taarifa kwenye ukurasa huo wa rais.

"Rais anaandika mwenyewe taarifa zake kwenye ukurasa wake. Ukiangalia katika siku za hivi karibuni mtandao wa facebook umechangia maamuzi anayopitisha. Kwa mfano suala la kulipiga marufuku shirikisho la soka nchini, NFF, lisishiriki kwenye mashindano ya kimataifa. Rais alibatilisha uamuzi wake kutokana na maoni yaliyoandikwa kwenye ukurasa wake na Wanigeria."

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, haandiki tu kuhusu soka bali pia juu ya mada ambazo zimeyafanya maisha ya Wanigeria kuwa magumu. Kwa mfano uzalishaji hafifu wa umeme au matatizo ya kimazingira katika eneo la mafuta la Niger Delta. Na Wanigeria wanaendeleza majadiliano. Kwa kila taarifa anayoiandika rais Jonathan kwenye ukurasa wake wa facebook, watu kati ya 1,500 na 2,000 huchangia maoni yao kwa haraka.

Katika mkahawa wa intaneti huko Sokoto kijana huyu Abdurrahman Mohammed anafurahia fursa hii mpya kwenye mtandao huo.

"Nimefungua ukurasa wangu binafsi kwenye tovuti ya facebook kwa sababu nimeona jinsi watu wengi uliwenguni wanavyoitumia tovuti hii. Kupitia facebook naweza kutoa maoni yangu na natumai kwa njia hii naweza kuchangia ili mambo mengi yabadilike nchini mwangu na ulimwenguni kote kwa jumla. Ni vyema kwamba rais wetu naye ameingia katika uwanja huu wa facebook. Ni jambo zuri sana kwa Wanigeria wote."

Sio wanasiasa na wananchi nchini Nigeria ambao wanautumia mtandao huu wa kijamii wa facebook. Hata maimamu sasa nao wako mbioni kujaribu kutafuta wafuasi kupitia facebook. Imamu Usman Aliyu anasema ameamua kutumia mtandao huu kuwahamasisha vijana kuhusu masuala ya dini na maadili mema kwa sababu ni wengi wanaoutumia.

Mwandishi: Awal Mohammad/ (DW Hausa)/Josephat Charo

Mhariri:Abdul-Rahman